Dar es Salaam. Baada ya kilio cha muda mrefu cha wastaafu wakilalamikia nyongeza ya pensheni, hatimaye Serikali imetangaza kiwango cha malipo hayo kwa mwezi kuanzia Januari 2025 kwa kuwapa nyongeza ya Sh50,000.
Nyongeza hiyo itafanya kiwango cha kima cha chini cha pensheni kutoka Sh100,000 hadi Sh150,000 huku wale waliokuwa wakipokea pensheni kuanzia Sh150,000 wataongezewa asilimia mbili.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema hayo leo Jumatano, Novemba 20, 2024 wakati wa kuhitimisha semina ya wastaafu watarajiwa wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Akizungumzia hatua hiyo Mainda Semfuko ambaye ni mnufaika wa pensheni amesema licha ya uamuzi huo kufanyika kwa kuchelewa, umekuja wakati muafaka hasa kipindi hiki ambacho gharama za maisha zimekuwa zikipanda siku hadi siku.
“Kwa kweli tumelalamika kwa muda mrefu na tulitarajia hili lifanyike mwaka huu lakini inaonekana mambo hayakukaa vizuri, sio mbaya hata kama itaanza mwakani Mungu akitupa uhai tutashukuru kwa sababu itatupunguzia makali ya gharama za maisha. Ukishakuwa mstaafu hauna kingine cha kutegemea zaidi ya pensheni,” amesema Mainda.
Mbali na hilo, Ridhiwani amesema kuanzia Januari 2025 mstaafu yeyote anayepokea pensheni PSSSF akifariki dunia familia yake itapata Sh500,000 kwa ajili ya maziko na wategemezi wake wanaotambulika watalipwa mkupuo wa miezi 36 wa pensheni ya mwezi ya mstaafu husika.
“Utaratibu huu ulishaanza tangu Julai 2022 lakini ulikuwa unatumika kwa wastaafu waliokuwa wanalipwa kwa kikokotoo kipya, lakini sasa utaratibu huu unafunguliwa kwa wastaafu wote hadi wale waliolipwa kwa kutumia vikokotoo vya zamani vya kwenye mifuko iliyounganishwa,” amesema Ridhiwani.
Kufuatia hilo amewaelekeza watendaji wa mfuko huo kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha wanufaika kupata haki yao pindi utekelezaji wa maelekezo hayo utakapoanza Januari 2024.
Mkurugenzi Mtendaji wa PSSSF, Abdul-Razaq Badru amesema tangu kuanzishwa kwa mfuko huo Sh10.4 trilioni zimelipwa kwa wanufaika 310,458 huku katika mwaka wa fedha 2024/2025 lengo likiwa kulipa pensheni na mafao mengineyo kwa wanufaika 11,622 yenye thamani ya Sh560 bilioni.
“Tunafarijika kwamba mfuko unaendelea kuimarika na unaendelea kuwa na uwezo wa kutimiza majukumu yake ikiwamo kulipa mafao ya wanufaika mbalimbali ikiwamo pensheni. Ndiyo maana nina kila sababu ya kukuhakikishia waziri kwamba mfuko uko hai na unaishi.
Semina za aina hii zinatusaidia kutuunganisha na wastaafu watarajiwa na inatufanya sisi kama mfumo tuendelee kuwa imara na kutimiza majukumu yetu kwa sababu tunalo jukumu la kuendelea kuhudumia wanufaika wengi ambao wanapata mafao mbalimbali,” amesema Badru.