Shirika la kimataifa la Air France laanza safari zake KIA,Naibu Waziri ashuhudia

Shirika la ndege la Air France limeanzisha rasmi safari zake kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwenda moja kwa moja Ufaransa (Charles de Gaulle) kuanzia tarehe 18 Novemba, 2024. Safari hizi zitafanyika mara tatu kwa wiki, kila Jumatatu, Jumatano, na Jumamosi. Shirika hili, ambalo ni miongoni mwa mashirika makubwa zaidi ya ndege barani Ulaya, litafanya safari zake kwa mtindo wa pembetatu, likianzia Ufaransa (Charles de Gaulle), kupitia Zanzibar, kisha KIA, na kurudi moja kwa moja Ufaransa. Safari hizi zitafanywa kwa kutumia ndege yake mpya aina ya Airbus A350-900WXB, yenye teknolojia ya kisasa na ufanisi wa hali ya juu.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa safari hizo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mh. David Kihenzile, alisisitiza umuhimu wa kuitumia vizuri fursa hii mpya ya safari za Air France, akibainisha kwamba itachangia kufungua milango ya kibiashara kati ya Tanzania na Ufaransa, pamoja na kuchochea ukuaji wa sekta ya uchumi na utalii.

Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Inj. Rehema Myeya amesema

“Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ipo tayari kabisa kwa ujio huu wa safari mpya za Air France. Tumekuwa tukihakikisha kuwa miundombinu yetu inakidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Pia, tumejipanga kutoa huduma bora kwa abiria wote ili waendelee kufurahia safari zao pindi wanapotumia viwanja vyetu vya ndege nchini”

Uzinduzi huu wa safari mpya za Air France ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kukuza nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki.

 

Related Posts