Siri muungano wa upinzani kushinda uchaguzi Mauritius

Kiongozi wa upinzani nchini Mauritius, Navin Ramgoolam ameibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge nchini humo.

Yeye na muungano wake wa Alliance of Change (ADC), walipata ushindi wa asilimia 62.6 ya kura na kumpatia nafasi ya kuwa Waziri Mkuu kwa mara ya nne.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Taifa la Mauritius (Mauritius Broadcasting Corporation), ADC ilishinda viti 60 kati ya 62 katika Bunge la Taifa.

“Mahakama ya wananchi imetoa uamuzi wake na Mauritius mpya imezaliwa,” alisema Ramgoolam, mwenye miaka 77 mbele ya umati wa wafuasi wake, huku wakishangilia kwa vifijo na honi za magari.

Ramgoolam aliwahi kuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1995 hadi 2000 na tena kati ya 2005 na 2014.

Mbali na viti 60 vya Mauritius, viti viwili viligombaniwa katika kisiwa cha Rodrigues, huku viti vingine vinane vikigawiwa kupitia mfumo wa kinachoitwa “best loser.” Waziri Mkuu aliyepo madarakani, Pravind Jugnauth, Jumatatu iliyopita alikubali kushindwa akisema muungano wake wa Lepep, unaoongozwa na chama chake cha Militant Socialist Movement (MSM), ulikuwa “ukielekea kushindwa vibaya…Wananchi wamechagua timu nyingine kuongoza taifa,” alisema Jugnauth, mwenye umri wa miaka 62, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Mauritius Novemba 10, 2024, uliitishwa baada ya serikali kufikia makubaliano na Uingereza kumaliza mzozo wa Visiwa vya Chagos.

Hata hivyo, siku chache kabla ya uchaguzi, kashfa ya kudukua mawasiliano kwa siri (wire-tapping) ilizuka.

Serikali ilijibu kashfa hiyo kwa kupiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii, marufuku ambayo ilitarajiwa kuendelea hadi baada ya uchaguzi. Hata hivyo, baada ya shinikizo la umma, marufuku hiyo iliondolewa siku moja baadaye. Muungano ulioshiriki uchaguzi ni pamoja na Alliance Lepep chini ya Waziri Mkuu Pravind Jugnauth na Alliance du Changement inayoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Navin Ramgoolam.

Masuala muhimu ya kampeni yalijikita katika gharama ya maisha, uhalifu na ufisadi. Jumla ya wapigakura 1,002,857 waliojiandikisha walistahili kupiga kura. Novemba 11, kura zilihesabiwa ambapo asilimia 79 ya wapigakura walijitokeza.

Alliance du Changement ilishinda uchaguzi huo kwa kishindo, ikinyakua majimbo 20 kati ya 21 ya nchi hiyo. Jugnauth alikubali kushindwa muda mfupi baada ya kuanza kwa mchakato wa kuhesabu kura.

Huu ulikuwa ushindi mkubwa zaidi tangu mwaka 1995. Wagombea wanne ambao hawakufanikiwa waliteuliwa kupitia ‘Mfumo wa Waliopata Nafasi Bora’ (Best Loser System), wawili kutoka Alliance Lepep na wawili kutoka Alliance Liberation.

Kutokana na mfumo wa upigaji kura wa ‘plurality block voting’, idadi ya kura zilizopigwa ilizidi jumla ya wapigakura waliosajiliwa.

Katika uchaguzi wa dharura wa mwaka 2019, Muungano wa Mauritian Alliance, ukiongozwa na Waziri Mkuu Pravind Jugnauth, ulishinda kwa kujipatia viti 42. Muungano wa Upinzani wa National Alliance, unaoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani Navin Ramgoolam, ulipata viti 17. Oktoba 2024, kashfa ya kudukua mawasiliano kwa siri ilizuka, ambapo mawasiliano ya simu ya waandishi wa habari, wanasiasa, wanachama wa mashirika ya kijamii na wanadiplomasia wa kigeni yalidukuliwa na kusambazwa mtandaoni.

Waziri Mkuu Jugnauth na Jeshi la Polisi la Mauritius walidai kuwa mawasiliano hayo yaliyovuja yalitengenezwa na teknolojia ya akili mnemba (AI). Hata hivyo, waandishi wa habari walioathiriwa na kitendo hicho walisema mawasiliano hayo yalikuwa halisi. Mwandishi mmoja alidai kuwa madai ya serikali kuhusu AI yalikuwa njia ya kupotosha umma kuhusu athari za kashfa hiyo.

Jugnauth alitangaza kuundwa kwa kamati ya dharura ili kuchunguza uvujaji huo. Kwa kuzingatia masuala ya usalama wa taifa, serikali ilipiga marufuku ya matumizi ya mitandao ya kijamii kuanzia Novemba 1, marufuku ambayo ilitarajiwa kudumu hadi siku moja baada ya uchaguzi.

Siku hiyo hiyo, washukiwa wanne, wakiwamo Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Mauritius Telecom, walikamatwa. Upinzani ulidai kuwa marufuku hiyo ilikuwa na nia mbaya ya kisiasa na ililenga kuzuia kushindwa kwa serikali ya Jugnauth katika uchaguzi.

Baada ya malalamiko makubwa kutoka kwa umma, serikali iliondoa marufuku hiyo kesho yake, Novemba 2.

Bunge la Kitaifa lina jumla ya wajumbe 62 waliochaguliwa moja kwa moja; 60 wanawakilisha majimbo 20 yenye viti vitatu kila moja, na wawili wanawakilisha jimbo la kisiwa cha Rodrigues.

Uchaguzi hufanyika kwa kutumia mfumo wa ‘plurality block vote’, ambapo mpigakura ana idadi ya kura sawa na viti vinavyopatikana. Kupitia mfumo unaojulikana kama ‘Best Loser System’, endapo jamii fulani itashindwa kupata uwakilishi bungeni, Tume ya Kusimamia Uchaguzi inaweza kuteua hadi wagombea wanane waliopata kura nyingi zaidi kutoka jamii hizo.

Tume ya Uchaguzi hugawa wapiga kura katika makundi manne: Wahindu, Waislamu, Wachina wa Mauritius na jamii ya jumla, ambayo inahusisha wapiga kura wasio wa makundi matatu ya kwanza. Isipokuwa Rais avunje Bunge la Kitaifa kabla ya muda wake, wajumbe hutumikia kipindi cha miaka mitano. Wagombea na wapiga kura wanaostahili lazima wawe na umri wa miaka 18 au zaidi, wawe raia wa Jumuiya ya Madola, na wawe wameishi Mauritius kwa angalau miaka miwili kabla ya tarehe ya uteuzi wa wagombea.

Tarehe ya mwisho ya uteuzi wa wagombea ilikuwa Oktoba 22. Jumla ya vyama 73 vilisajiliwa kushiriki uchaguzi huo. Miungano miwili mikubwa ilitangaza kushiriki uchaguzi huo: Alliance Lepep, iliyoanzishwa mwaka 2014 na kuongozwa na Waziri Mkuu Pravind Jugnauth, na Alliance du Changement ya Navin Ramgoolam, iliyoanzishwa muda mfupi kabla ya tarehe ya uteuzi wa wagombea.

Mbali na Militant Socialist Movement ya Jugnauth, vyama vingine vinavyounda Alliance Lepep ni Parti Mauricien Social Democrate’, ‘Muvman Liberater’, ‘Plateforme Militante’, na ‘Muvman Patriot Morisien’.

Vyama vinavyoshirikiana na ‘Alliance du Changement’ ni ‘Labour Party’ ya Ramgoolam, ‘Mauritian Militant Movement’ ya Waziri Mkuu wa zamani Paul Bérenger, ‘Rezistans ek Alternativ’, na ‘New Democrats’.

Jumla ya wagombea 891 walishiriki katika uchaguzi huo. ‘Alliance Lepep’ na ‘Alliance du Changement’ kila moja ilisimamisha wagombea 60.

Kulikuwa na wagombea huru 514, huku wagombea waliobaki wakihusishwa na vyama vingine au miungano. Ni wagombea 165 pekee waliokuwa wanawake, wakati wagombea 273 walikuwa na umri wa chini ya miaka 40. Kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa 2019, ‘Rodrigues People’s Organisation’ ilishiriki tu katika jimbo la kisiwa cha Rodrigues.

Related Posts