Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
MAMLAKA ya Maendeleo ua Biashara Tanzania (TANTRADE) imezindua shindano la ubunifu wa logo ya ‘Made in Tanzania’ ambapo kazi za wasanii mbalimbali zitashindanishwa kwa lengo la kupata nembo ambayo itaitambulisha Tanzania katika bidhaa mbalimbali hasa zinasafirishwa nje ya nchi.
Akizungumza leo Novemba 20, 2024 Mkurugenzi wa Mkuu wa Tantrade Latifa Khamis amesema shindano la logo ya ‘Made in Tanzania’ ni muhimu kwa wasanii wa Kitanzania ambapo lina lengo la kutambulisha bidhaa zenye asili ya Kitanzania katika masoko ya Kimataifa.
“Shindano hili linatoa jukwaa la kipekee kwa wabunifu wa picha na wasanii wa Tanzania katika kuunda utambulisho wa taifa letu na kuonyesha bunifu, fahari, na uwezo ulio ndani ya bidhaa na huduma zetu za ndani.
“Lengo la shindano hili ni kuunda logo inayotambulika na ya kipekee ambayo itakuwa Nembo ya Taifa letu. Logo hii itawakilisha kwa fahari bidhaa na huduma za Tanzania hapa nchini na kimataifa, na kuwa alama ya ubora, imani, na fahari,lengo letu ni kuhakikisha kuwa bidhaa za Tanzania zinafahamika zaidi,”alisema Latifa.
Amesema Tanzania imefanya maendeleo makubwa katika kuongeza mwonekano wake duniani na kuboresha uhusiano wake wa kibiashara.
“Licha ya mafanikio yetu mengi,kumekosekana kipengele kimoja,ishara ya taifa inayounganisha na kuwakilisha ubora na upekee wa bidhaa na huduma za Tanzania katika soko la kimataifa,hapa ndipo shindano la Logo ya Made in Tanzania linapolenga kutoa suluhisho.
Amesema utambulisho wa logo utakuwa utambulisho wenye nguvu wa chapa utaimarisha ushindani wetu, kuongeza mahitaji ya bidhaa na huduma za Tanzania, na kuvutia wawekezaji katika uchumi wetu.
“Nawaalika wabunifu wa picha na wasanii, kutoka mikoa yote ya Tanzania kushiriki katika shindano hili la kihistoria,hii ni nafasi yenu ya kuacha alama ya kudumu kwenye mustakabali,”alisema Latifa.
Amesema mwisho kuwasilisha kazi hizo ni Novemba 24 mwaka huu ambapo mshiriki ataruhusiwa kukusanya bunifu zisizochini tati.
Akizungumzia zawadi watakazopata wabunifu hao alisema mshindi wa kwanza atapata Tsh 3,000,000, mshindi wa pili atapata Tsh 2,000,000, na mshindi wa tatu atapata Tsh 1,500,000.