Trump kutimua wahamiaji Wakenya 30,000 Marekani?

Washington. Zaidi ya Wakenya 30,000 wanaoishi nchini Marekani bila vibali halali wanakabiliwa na hatari ya kufukuzwa, kutokana na mipango ya utawala wa Rais mteule Donald Trump kuimarisha usalama wa mipaka na kuchukua hatua kali dhidi ya wahamiaji haramu.

Kwa mujibu wa taarifa za kituo cha televisheni cha NDTV cha India, Trump amedhamiria kutangaza hali ya dharura ya kitaifa kuhusu usalama wa mipaka, hatua inayolenga kuziba mianya inayoruhusu wahamiaji kuingia na kuishi nchini humo kinyume cha sheria.

Mpango huu pia unahusisha kutumia vikosi vya kijeshi kusaidia utekelezaji wa sera za uhamiaji, jambo ambalo limeibua mjadala mkali nchini Marekani.

Kutekeleza mpango huo, Trump ameanza kuteua viongozi wenye misimamo mikali kuhusu uhamiaji kushika nafasi muhimu katika Serikali yake, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha ahadi zake za kampeni kuhusu uhamiaji zinatimizwa.

Hatua hizi zimezua hofu miongoni mwa wahamiaji kutoka mataifa mbalimbali, wakiwemo Wakenya wanaoishi Marekani bila vibali halali.

Trump, ambaye ni miongoni mwa viongozi wanaotumia sana mitandao ya kijamii, Novemba 18, alichapisha tena ujumbe kupitia ukurasa wa X (zamani wa Twitter) wa mshirika wake, Tom Fitton ambaye ni mkuu wa shirika la uangalizi wa masuala ya kisheria.

Fitton alidai utawala mpya umejipanga kutumia jeshi kutekeleza operesheni hiyo, hasa kwa wahamiaji haramu kutoka Afrika waliovuka mipaka kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Sensa ya Marekani ya mwaka 2020, kuna jumla ya wahamiaji haramu milioni 11 nchini Marekani, wakiwemo Wakenya 30,000. Idadi hiyo inatarajiwa kuwa kubwa zaidi mwaka 2024.

Marekani inahifadhi idadi kubwa ya wahamiaji wa Kenya (157,000), ikifuatiwa na Uingereza (139,000), na Kenya inashika nafasi ya tano kati ya nchi za Kiafrika zenye wahamiaji wengi Marekani, huku nchi ya Nigeria ikishika nafasi ya kwanza.

Hatua ya Trump imeongeza hofu ya kufukuzwa kwa Wakenya hao, wengi wao wakiwa wameishi Marekani kwa miaka mingi na kujenga maisha yenye heshima.

Mbali na hilo, tishio lingine linalozua wasiwasi ni mabadiliko yanayoweza kuathiri mpango wa Mafunzo ya Hiari kwa Vitendo (OPT).

Programu hii huwapa wanafunzi wa kimataifa fursa ya kupata uzoefu wa kazi katika taaluma zao kwa hadi miaka mitatu baada ya kuhitimu.

Wakati wa muhula wake wa kwanza baada ya uchaguzi wa 2016, Trump alifikiria kuweka vikwazo kwenye OPT, hasa kwa wanafunzi wa fani za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).

Hatua kama hiyo sasa inatishia mustakabali wa wanafunzi wa Kenya wanaotegemea mpango huo.

Ili kufanikisha azma yake ya kupunguza uhamiaji haramu, Trump amewateua maofisa wenye msimamo mkali kushika nyadhifa muhimu, akiwemo Gavana wa Dakota Kusini, Kristi Noem, ambaye anasubiri kuthibitishwa na Seneti kuwa Waziri wa Usalama wa Ndani.

Kwa sasa, wahamiaji wa Kiafrika, wakiwemo Wakenya, wanasubiri kwa tahadhari kuona namna sera kali za uhamiaji za Trump zitakavyotekelezwa.

Tishio hili linaweka hatma ya maelfu ya Wakenya kwenye hali ya wasiwasi mkubwa.

Related Posts