TUNA MTAJI WA IMANI YA WATANZANIA: NCHIMBI

-Azindua kampeni Mwanza akitamba na takwimu za kura za uhakika

-Awasihi wanaCCM kila mmoja kutafuta kura 10 kwa ajili ya ushindi wa kishindo

-Ahamasisha kampeni za nyumba kwa nyumba na mtu kwa mtu, isiachwe kura hata moja, wakiwemo wapinzani

-Awataka washindi kuwatumikia Watanzania kwa kupinga dhuluma na rushwa

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesema CCM inaingia kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa kikiwa na imani kubwa ya Watanzania kutokana na uimara wa chama na uongozi wa Mwenyekiti wake, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema kuwa uimara wa CCM unatokana na wingi na umakini wa wanachama wake, akitoa takwimu jinsi wanachama wapatao milioni 8 wa CCM walivyojitokeza kupiga kura wakati wa mchakato wa ndani ya chama hicho kupata wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Balozi Nchimbi amesema mtaji wa imani ya Watanzania, utumishi wa CCM kupitia sera zake, na uongozi makini unakipatia chama hicho uhakika wa ushindi mkubwa wa kishindo katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024.

Katibu Mkuu huyo wa CCM aliyasema hayo alipokuwa akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za CCM kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Mkoa wa Mwanza, uliofanyika katika Viwanja vya Furahisha, jijini Mwanza, leo tarehe 27 Novemba 2024.

Katika kujihakikishia ushindi huo wa kishindo, Balozi Nchimbi alisisitiza kampeni za kuomba kura ziwalenge hata wanachama na viongozi wa vyama vya upinzani, ili kuhakikisha kila kura inapatikana kwa ajili ya CCM, akiwahamasisha kupiga kampeni “nyumba kwa nyumba na mtu kwa mtu” nchi nzima.

“Pamoja na uhakika wa kura, msiridhike na ushindi. Twendeni nyumba kwa nyumba na mtu kwa mtu. Tusiache kura hata moja. Kila mwanachama atafute kura 10. Hata wa vyama vya upinzani, wawe ACT, NCCR, Chadema, na wote, watatupigia kura. Tumalizeni huu mchezo kwa kuipatia CCM ushindi mkubwa wa kishindo.

“Wajibu wetu ni kuwakumbusha tu Watanzania kazi kubwa ambayo CCM imeendelea kufanya katika kutoa uongozi wa nchi hii. Uhakika wa kesho ya Tanzania uko CCM. Watanzania wana imani kubwa na CCM kila wanapofikiria maendeleo, umoja wa nchi yetu, utaifa wetu, amani na utulivu. Tunataka wagombea wetu mtakapochaguliwa mkalinde heshima na imani hii ya Watanzania kwa kuwatumikia vizuri, mkijiepusha na dhuluma na rushwa,” alisema Balozi Nchimbi.

Aidha, akisisitiza kuhusu uimara wa CCM, Balozi Nchimbi alisema CCM ndiyo chama pekee ambacho wanachama wake, kwa mamilioni, walijitokeza kushiriki mchakato wa ndani wa kupata wagombea, hasa kupitia kura za maoni. Hii ndiyo sababu kimesimamisha wagombea maeneo yote nchi nzima katika uchaguzi huo, kwa kuwa kimeenea nchi nzima, tofauti na vyama vingine vya upinzani.






Related Posts