UDART wachangia maji ya Afiya katoni 500 uokoaji Kariakoo

Kampuni ya Mabasi yaendayo Haraka (UDART) imeungana na juhudi za kusaidia waathirika wa ajali ya kuanguka kwa jengo la ghorofa nne lililotokea hivi karibuni eneo la Kariakoo. Katika kuonyesha mshikamano wa kijamii, UDART imetoa msaada wa katoni 500 za maji ya kunywa kusaidia timu za uokoaji na waathirika wa tukio hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa UDART, akiwa ameambatana na viongozi wengine wa kampuni hiyo, alifika eneo la tukio kutoa msaada huo na kuonyesha mshikamano na waathirika pamoja na timu zinazofanya kazi ya uokoaji.

Akizungumza wakati wa kutoa msaada huo, Mkurugenzi Mkuu wa UDART alisema, “Tumesikitishwa sana na tukio hili, na tumeona ni muhimu kushiriki kwa vitendo katika juhudi za kusaidia wale walioathirika. Kama kampuni inayohudumia jamii, ni wajibu wetu kuwa pamoja katika nyakati za dharura kama hizi.”

Timu za uokoaji, maafisa wa serikali, na wananchi walipokea msaada huo kwa shukrani, wakieleza kuwa mchango huo umesaidia kuimarisha juhudi za uokoaji zinazoendelea.

Wanajamii na mashirika mengine wamehimizwa kuiga mfano wa UDART kwa kuendelea kutoa msaada kwa waathirika na wanaojitahidi kuokoa maisha katika tukio hili la kusikitisha. Shughuli za uokoaji bado zinaendelea, huku matumaini ya kuokoa maisha zaidi yakiwa juu.

Related Posts