Dar es Salaam. Saa 11.00 alfajiri alikuwa amejiandaa kikamilifu kutimiza nia yake mbaya ya kuiba mtoto hospitalini jambo analojutia na kuwaonya wanawake kuwa na subira maishani.
Lengo lake kubwa alitaka kuwa mama kwa gharama yoyote baada ya miaka mingi ya vipigo katika ndoa zake mbili zilizovunjika.
Katika moja ya matukio ya vipigo, alikaa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kwa siku mbili.
Hivi ndivyo Mwenyekiti wa Chama cha Wagumba Tanzania, Shamila Makwenjula, anavyoanza kusimulia hali yake ya kutokuwa na uwezo wa kupata watoto ilivyoathiri maisha yake na kusababisha afikie uamuzi mbaya, lakini baadaye aliamua kuanzisha chama cha kuhamasisha jamii kuhusu suala hilo na kupinga unyanyapaa unaohusiana nalo.
Mwaka 2018, daktari alimwambia rasmi kuwa asingeweza kupata watoto kutokana na ugumba, ambayo ni hali ya mwanamume au mwanamke kutokuwa na uwezo wa kuzaa licha ya kufikia umri wa kuweza kufanya hivyo.
“Niliathirika kisaikolojia. Licha ya kupigwa sana na mume wangu, bado nilitaka kupata mtoto na heshima kutoka kwa jamii ambayo sikuwa nayo kwa miaka mingi. Nilihama kutoka Malinyi, Morogoro kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi, hapo ndipo nilipomdanganya mume wangu kuwa nilikuwa mjamzito,” anasema.
Alijifanya kuwa na ndugu mgonjwa, akilini mwake alipanga kuiba mtoto yeyote asiyeangaliwa vizuri wodini. Hata hivyo, hakufanikisha hilo, mwishowe akakata tamaa.
Hali hiyo ilimfanya amuulize muuguzi jinsi ya kupata mtoto, akaishia kutukanwa na muuguzi huyo.
“Niliondoka wodini nikiwa nimekata tamaa. Mungu ashukuriwe, nilipofika nje ya lango la hospitali niliona mwanamke aliyekuwa amebeba mtoto mdogo akiwa pekee, huku amebeba mizigo. Nilijitolea kumsaidia kubeba mtoto huku nikimuuliza kwa nini yuko peke yake.
Alijibu ndugu zake hawakufika na alikuwa amesharuhusiwa kurudi nyumbani.
Anasema alimsaidia mwanamke huyo kurudi nyumbani kwa mpango wa kuiba mtoto.
Walipokuwa wakielekea kwenye basi, mwanamke huyo aliitwa na daktari kuchukua dawa alizosahau kwa ajili ya mtoto wake, hivyo Shamila akabaki na mtoto.
“Huo ndiyo ulikuwa muda wangu. Nilitembea hatua mbili nikiwa na mtoto, lakini nikasita na kuanza kulia, nikifikiria nini kingetokea kwa mtoto mgonjwa ambaye hata dawa zake sikuwa nazo. Nilianza kulia kwa sauti kubwa, huku nikitetemeka. Wakati watu walikuwa wanashangaa, mama huyo alitokea na kuninyang’anya mtoto wake,” anasema.
Mama huyo alishangaa ni kwa nini nilikuwa nalia huku nikiwa nimemshika mwanaye. Alifoka kisha akamchukua na mwanaye, ambaye awali alinieleza kuwa alikuwa mgonjwa tangu alipozaliwa.
Niliondoka pale na kurudi nyumbani bila mtoto, huku nikiwa nimechanganyikiwa.
Anaeleza alipitia changamoto za afya ya akili na bado anakabiliana nazo, lakini amekuwa akihudhuria kliniki kwa muda mrefu sasa.
Anaeleza imekuwa ni utaratibu wake kwa sababu watu wenye tatizo la ugumba wanahitaji matibabu hayo katika maisha yao.
“Tunakumbana na unyanyapaa katika jamii kiasi kwamba hata hatuaminiki kuwa viongozi wazuri katika jamii, hatupewi nafasi ya kutoa maoni kwenye mikutano ya kifamilia, na wengi wanadhani hatupaswi kufanya kazi kwa bidii au kumiliki mali kwa sababu hatuna watoto,” anasema.
Katika juhudi za kutafuta mtoto, Shamila anasema aliamua kutumia waganga wa kienyeji waliompa mitishamba mingi, na baadhi ilimdhuru kiafya kwani aliiingiza ukeni.
Hali haikuishia hapo, anasema aliwahi kuambiwa na mganga mmoja ale chakula chooni na kutupa sehemu ndogo ya chakula ndani ya choo kama ishara ya kutupa tatizo lake la ugumba.
Mbali ya hilo, alitakiwa kunywa dawa za kienyeji zilizochemshwa kwenye msiba wakati mwili wa marehemu ukitolewa nyumbani, akiaminishwa mwili huo ungeondoka na tatizo lake la ugumba.
Katika mwaka wa 10 ndani ya ndoa yake ya pili, mume wake alipata mtoto na mwanamke mwingine. Hilo kwake lilikuwa adhabu, akieleza mwanamke huyo alipata upendeleo akiruhusiwa kutumia chochote ndani ya nyumba yao licha ya kuishi eneo tofauti.
Ilikuwaje akaishia ICU? Anaeleza tukio lililompeleka huko ni la mwanamke huyo kumtuma mtu kuchukua baiskeli nyumbani kwa ajili ya kwenda kufuata maji ya kufua nguo za mtoto.
“Kwa kuwa mimi na mume wangu tulikuwa na baiskeli, nilikataa baiskeli yangu isitumiwe na mwanamke huyo kwa sababu nilikuwa nakwenda nayo sokoni. Mume wangu alinikasirikia, akisema mimi ni mchoyo na sijali kuhusu mtoto. Alianza kunipiga, nilipozinduka nilijikuta ICU na niliambiwa nilikuwa pale kwa siku mbili,” anaeleza.
Anasema baada ya kugundua hataweza kupata watoto, aliamua kuanzisha Chama cha Watu wenye Ugumba Tanzania (CCWT) mwaka 2015.
Chama hicho anasema kilisajiliwa mwaka 2022, baada ya kuwa kimeanza kama kikundi cha wanawake 15 kikiitwa Wangalela kwa lugha ya Kipogoro, ikimaanisha watu wasio na watoto.
“Kujua kuwa hutawahi kuwa na watoto milele ni jambo la kuumiza sana na halisahauliki. Mioyo yetu daima haijatulia. Jamii inapaswa kuacha kutuita majina mabaya. Kutokuwa na watoto peke yake ni zaidi ya maumivu ya kutosha,” anasema.
Anasema chama hicho hivi sasa kina wanachama 437 nchi nzima, ambao wanapigania haki zao wakipinga kunyanyaswa na kunyimwa haki zao kutoka kwa wenzi wao kwa sababu tu hawana watoto.
Ameomba msaada kutoka kwa watu mbalimbali kusaidia gharama za matibabu na kuelimisha jamii kuwa ugumba ni ugonjwa unaowakumba wanaume na wanawake, huku wanaume wengi hawajitokezi kwa sababu ya kuogopa unyanyapaa.