Waathirika jengo Kariakoo kupoteza mamilioni ya fidia

Dar es Salaam. Waathirika na ndugu wa walioathiriwa na kuporomoka jengo la ghorofa nne Kariakoo wangelipwa mamilioni ya fidia iwapo Sheria ya Bima, Sura ya 394, ingetekelezwa kikamilifu, wachambuzi wanasema.

Serikali ilibadilisha Sheria ya Bima, Sura ya 394, kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2022, ili kupanua bima ya lazima kujumuisha masoko ya umma, majengo ya kibiashara, bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na meli.

Hata hivyo, tangu wakati huo, sheria hiyo haijatekelezwa kutokana na ukosefu wa kanuni za kuisimamia.

Jumamosi, Novemba 16, 2024 jengo la ghorofa nne liliporomoka eneo la biashara la Kariakoo na hadi leo Jumatano, Novemba 20, 2024 saa 3 asubuhi watu 20 walikuwa wamefariki dunia, huku wengine 88 wakiokolewa.

Ofisa Mwandamizi wa Sheria wa Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (Tira), Jamali Mwasha, ameliambia gazeti dada la The Citizen leo Novemba 20, kuwa sheria hiyo bado haijaanza kutumika kwa sababu inahitaji waziri kuandaa kanuni zinazoelezea mali zinazopaswa kuwekewa bima na aina za bima zinazohusika.

Amesema rasimu ya kanuni ipo tayari, na juhudi zinaendelea kupanua wigo wa maoni ya umma ili kuzilinganisha na mbinu bora na kuhakikisha zinakidhi mahitaji ya watu.

“Kampeni za uhamasishaji zimefanyika kupitia vyama na taasisi, na sasa tunakamilisha maoni ya mwisho, ambayo yanalenga zaidi sekta binafsi,” amesema.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Wizara ya Fedha, Ben Mwaipaja amesema angezungumzia suala hilo kwa kushauriana na idara husika ili kubaini hatua iliyofikiwa.

Mtaalamu wa bima na aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Bima (Ati), Khamis Suleiman amesema hakuna fidia ya bima itakayotolewa kwa sababu sheria haijaanza kutekelezwa licha ya kufanyiwa mapitio mwaka 2022.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza alipotembelea jengo la ghorofa lililoporomoka Kariakoo.

Amedai ucheleweshaji uko kwa Serikali, kwani Tira imeshashughulikia suala hilo. Kinachohitajika sasa ni mfumo wa kutekeleza kanuni hizo, lakini bado haujatolewa.

“Kama hili halitafanyika, majanga yataendelea kutokea, na watu watateseka bila bima,” amesema.

Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kimataifa, Utafiti na Ushauri wa Chuo cha Afrika cha Bima na Ulinzi wa Jamii (ACISP), Dk Anselm Anselm amesema ingawa kuandaa sheria kunaweza kuchukua muda, maandalizi ya kanuni yanapaswa kukamilika ndani ya mwaka mmoja.

Dk Anselm amesema tathmini ilionyesha utekelezaji wa sheria hiyo unaweza kuwa na athari kubwa kwenye sekta ya bima. Kwa mfano, ada za bima kwenye majengo peke yake zinaweza kufikia Sh500 bilioni, sawa na asilimia 30 ya ada zote za bima. Kuongeza uelewa kutajenga imani na kuhamasisha watu kuchukua bima katika maeneo mengine.

“Tatizo letu ni kwamba tunachukua hatua haraka tu majanga yanapotokea. Sheria hii iliundwa baada ya matukio kama moto wa masoko, lakini tumesahau mpaka janga lingine linapotokea. Serikali inapaswa kukamilisha mchakato, kuandaa kanuni na kuanza utekelezaji,” amesema.

Kilio cha wafanyabiashara

Katika hatua nyingine, wafanyabiashara wenye maduka na vyumba vya kuhifadhi mizigo katika jengo hilo wameeleza wanangoja tamko la Serikali kuhusu hatima ya bidhaa zao zilizo kwenye kifusi.

Waathirika waliookolewa katika jengo la ghorofa lililoporomoka Kariakoo.

Leo Novemba 20, baadhi ya wafanyabiashara  wamekusanyika jirani na eneo la tukio baada ya kupokea taarifa kwamba Rais Samia Suluhu Hassan angefika kuzungumza nao.

“Mimi na wenzangu tumekuwa hapa tangu siku ya tukio na hatujarudi nyumbani. Tumeambiwa tumsubiri Rais, kwani yeye ndiye atakayeamua hatua za kuchukuliwa kuhusu jengo hili na bidhaa zetu,” amesema John Mafuru, mmoja wa wafanyabiashara walioathirika.

Amesema wapo pia wafanyabiashara ambao hawakuwa na maduka katika jengo hilo, bali walihifadhi mizigo hapo.

“Ni muhimu na wao kuwepo ili kujua nini kitafanyika,” anasema.

Hata hivyo, Rais Samia alipofika eneo hilo kuzungumza na kujione hali halisi amesema  vitu vilivyokuwa kwenye jengo hilo vitakusanywa, kisha utaratibu utaandaliwa ili kila muhusika apatiwe.

Related Posts