Wafanyabiashara jengo lililoporomoka Kariakoo wasubiri kauli ya Serikali

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wenye maduka na vyumba vya kuhifadhi mizigo katika jengo lililoporomoka Kariakoo wameeleza wanangoja tamko la Serikali kuhusu hatima ya bidhaa zao zilizo kwenye kifusi.

Ghorofa hilo liliporomoka Jumamosi saa tatu asubuhi ya Novemba 16, 2024 na kusababisha vifo vya watu 16 na majeruhi 88.

Uokoaji ambao kwa mujibu wa wataalamu ulipaswa kufanyika ndani ya saa 72, uliongezwa saa 24 kwa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan jana Novemba 19 hadi leo Novemba 20.

Rais Samia alimtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhakikisha uokoaji unaendelea kwa saa 24 zaidi, kwa matumaini ya kuwaokoa watu ambao huenda walikuwa hai chini ya kifusi.

Leo Novemba 20, baadhi ya wafanyabiashara  wamekusanyika jirani na eneo la tukio baada ya kupokea taarifa kwamba Rais Samia angefika kuzungumza nao.

“Mimi na wenzangu tumekuwa hapa tangu siku ya tukio na hatujarudi nyumbani. Tumeambiwa tumsubiri Rais, kwani yeye ndiye atakayeamua hatua za kuchukuliwa kuhusu jengo hili na bidhaa zetu,” amesema John Mafuru, mmoja wa wafanyabiashara walioathirika.

Amesema wapo pia wafanyabiashara ambao hawakuwa na maduka katika jengo hilo, bali walihifadhi mizigo hapo kwa ajili ya biashara zao kwenye mitaa mingine ya Kariakoo.

“Ni muhimu na wao kuwepo ili kujua nini kitafanyika,” anasema.

Taarifa za ujio wa Rais Samia zimeleta mabadiliko katika mitaa ya Kariakoo, maduka mengi yamefungwa huku ulinzi ukiimarishwa na usafi ukifanyika katika mitaa ya jirani.

Jana Novemba 19, maduka kadhaa yakiwemo ya katikati ya mitaa ya Nyamwezi na Congo, yalifunguliwa kwa muda kuruhusu shughuli za kibiashara.

Hata hivyo, kutokana na wingi wa watu mchana, biashara zilisitishwa.

Leo asubuhi Mwananchi imeshuhudia maduka mengi katika mitaa ya Kariakoo yakiwa yamefungwa, huku wateja wakihamishia shughuli zao kwenye maduka ya mtaa wa Narung’ombe kuelekea soko Kuu la Kariakoo.

Related Posts

en English sw Swahili