Wapemba waliobadili majina wahangaika kupata uraia wa Kenya

Mombasa. Baadhi ya watu wenye asili ya Pemba, Zanzibar wameeleza changamoto wanazokutana nazo katika mchakato wa kujisajili kuwa raia wa Kenya, licha ya hatua ya Rais William Ruto kuwapa uraia mwaka 2023.

Rais Ruto alitoa uraia kwa watu takribani 7,000 wa jamii hiyo waliokuwa wakiishi Kenya kwa zaidi ya miaka 100 bila utambulisho rasmi.

Uamuzi huo uliifanya jamii ya Wapemba kuwa moja ya makabila yanayotambuliwa rasmi na kuwaletea fursa ya kupata vibali muhimu kama vitambulisho vya kitaifa na vyeti vya kuzaliwa kwa ajili ya huduma za kijamii.

Hata hivyo, mchakato wa kurejea majina yao halisi umekuwa mgumu, hasa kwa wale waliobadilisha majina yao zamani ili kuepuka changamoto za kisheria.

Dida Hamadi Makame, mmoja wa wanajamii hiyo, amelieleza gazeti la Taifa leo la kenya, kuwa hawezi kurudi kwenye jina lake la asili baada ya kulibadilisha awe Dida Hamisi Idi mwaka 1986.

Naye Abdul Mohamed Mbarari, ambaye pia anatoka katika jamii hiyo, alisema kuna baadhi yao walipewa vitambulisho mwaka uliopita katika hafla iliyoongozwa na Rais Ruto mjini Kilifi, lakini hawawezi kuvitumia.

Naibu Katibu wa Wapemba nchini Kenya, Omar Kombo, amethibitisha akisema ingawa Serikali imeonyesha nia ya kutatua tatizo la uraia kwa jamii hiyo, kuna baadhi yao bado hawatambuliwi kuwa Wakenya.

“Jamii ya Wapemba itaendelea kukosa uraia ikiwa baadhi yetu bado hawatambuliwi,” alisema.

Ijumaa iliyopita, katika hafla ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu Wapemba wapewe uraia Kenya, Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Owen Baya alisema masaibu hayo yanasikitisha.

Aliiomba Serikali itume maofisa husika kuweka kambi katika maeneo ya Pwani ambako Wapemba hupatikana, ili kutatua hali hiyo.

“Tunataka suala hili litatuliwe mwaka huu ili ifikapo 2025, kusiwe na Mpemba yeyote ambaye atanyimwa huduma katika benki na pia waweze kujisajili kwa bima ya kijamii ya afya (SHIF),” alisema.

Katibu wa Uhamiaji na Huduma za Raia Julius Bitok, alitoa hakikisho kwamba Serikali imejitolea kuhakikisha Wapemba wanapokea huduma zote nchini, sawa na raia wengine wa Kenya.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuna Wapemba karibu 7,000 nchini Kenya huku Serikali ikisema kuna zaidi ya Wapemba 6,000 walishasajiliwa kuwa Wakenya rasmi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) liliipongeza Serikali ya Kenya kwa kutoa uraia kwa jamii wa watu wa Pemba ikiwa ni hatua madhubuti ya dhamira ya nchi ya kusaidia kuondoa tatizo la baadhi ya watu kukosa utaifa.

Rais Ruto alitoa vitambulisho vya utaifa, vyeti vya kuzaliwa na pasi za kusafiria kwa wanajamii wa Pemba ambao wamekuwa wakiishi nchini humo kwa miongo kadhaa wakiwa wametokea eneo la Pemba, Zanzibar nchini Tanzania.

Tukio hilo lilihitimisha mchakato wa uandikishaji wa wanajamii wote 7,000 wa Pemba na sasa watakuwa na fursa ya kupata huduma zote za kijamii ikiwemo elimu, afya, ulinzi wa kijamii, huduma za kifedha na ajira rasmi.

Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi alisema, “ninapongeza uongozi wa Serikali ya Kenya katika kushughulikia changamoto nyingi zinazowakabili watu waliohamishwa na kuchukua hatua muhimu za kutokomeza ukosefu wa utaifa katika nchi hii.”

Desemba 2022, Rais Ruto alitangaza kwamba Serikali yake itaanza kuwatambua rasmi Wapemba kama raia wa Kenya.

Uamuzi huu wa hivi karibuni ni maendeleo yanayokaribishwa na kupongezwa na Umoja wa Mataifa katika kujitolea kwa Serikali ya Kenya kutimiza ahadi zake katika sehemu ya ngazi ya juu ya kutokuwa na utaifa Oktoba 2019, ikijumuisha kujiunga na mikataba miwili ya Umoja wa Mataifa ya kutokuwa na utaifa.

Related Posts