Wawili kizimbani wakidaiwa kukwepa kodi ya TRA

Dar es Salaam. Wakazi wawili jijini hapa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakishtakiwa kwa makosa tisa yakiwamo ya kughushi nyaraka za kiwanja, kukwepa kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kutakatisha Sh54 milioni.

Washtakiwa hao ni Mohamed Awadhi (49) na Kassim Simba (56) wanaodaiwa kukwepa kodi ya TRA kwa kulipa Sh54 milioni baada ya kudanganya kiwanja kilichopo Kariakoo wamenunua kwa Sh190 milioni badala ya thamani halisi ya Sh900 milioni.

Awadhi mkazi wa Upanga na Simba, anayeishi Kipunguni B, wamefikishwa mahakamani leo Novemba 20, 2024 wanakokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.

Mashtaka yanayowakabili, matatu ni ya kughushi nyaraka, kuwasilisha nyaraka za uongo, kukwepa kodi na kutakatisha fedha.

Wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru amedai washtakiwa walitenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Machi 30 hadi Julai 30, 2014 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam. Upande wa mashtaka pia unawakilishwa na Wakili Aaron Titus.

Mafuru amedai washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kugushi, wakidaiwa kughushi nyaraka mbalimbali ikiwamo fomu ya ardhi namba 35 inayohusu kiwanja namba 9 kitalu namba 14.

Inadaiwa washtakiwa waligushi nyaraka hiyo wakionesha Mohamed Awadhi, amenunua kiwanja hicho kwa Sh190 milioni kutoka kwa wanafamilia wanne Kasim Yusuph, Ramadhani Yusuph, Fatuma Yusuph na Mwanahamisi Yusuph wakati wakijua si kweli.

Kwa tarehe hizo, wanadaiwa walighushi mkataba wa manunuzi wa Machi 20, 2014 wakionyesha Mohamed Awadhi amenunua kiwanja hicho, wakati si kweli.

Washtakiwa pia wanadaiwa kughushi ripoti ya tathmini ya ardhi wakijaribu kuonyesha tathmini iliandaliwa na Mamlaka ya Ardhi kupitia mtathmini daraja la tatu, Pili Ngobeka wakionyesha kuwa kiwanja hicho kina thamani ya Sh190 milioni.

Mafuru amedai Mei 14, 2014, katika Ofisi ya Usajili wa Hati iliyopo Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam waliwasilisha nyaraka za kughushi ambazo ni ripoti ya Tathmini ya Ardhi na fomu ya ardhi, huku mkataba wa mauziano wa kughushi wakiuwasilisha TRA.

Inadaiwa kati ya Machi 20 na Julai 30, 2014, katika ofisi za TRA, washtakiwa kwa nia ovu, katika mchakato wa kufanya uhamisho wa umiliki wa kiwanja hicho kilichopo Kariakoo waliipatia TRA hasara ya Sh54.8 milioni.

Inadaiwa kwa kitendo hicho, mshtakiwa Awadhi alikwepa kodi binafsi ya Sh54.8 milioni kwa kulipa kiasi kidogo cha kodi baada ya kudanganya kiwanja alinunua Sh190 milioni badala ya thamani halisi ya Sh900 milioni.

Katika shtaka la kutakatisha fedha, Mafuru anadai kati ya Machi 20 na Julai 30, 2014, katika ofisi za TRA na maeneo mengine, washtakiwa walijihusisha na muamala wa Sh54.8 milioni huku wakijua fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la ukwepaji kodi.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kisheria wa kusikiliza kesi hiyo.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi wa shauri hilo umekamilika, hivyo umeomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuwasilisha kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuruhusu Mahakama hiyo kusikiliza shauri hilo.

Hakimu Nyaki alikubali ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Desemba 3, 2024.

Washtakiwa wamerudishwa mahabusu kutokana na shtaka la kutakatishaji fedha kutokuwa na dhamana.

Related Posts