Yanga yapewa nondo za CAF

KWA sasa Yanga iko katika hatua muhimu kuelekea mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya mabingwa wa Sudan, Al-Hilal Omdurman. Katika kujiandaa kwa mchezo huo, wamevujishiwa mbinu na rafiki wa karibu wa kocha wa Al-Hilal, Florent Ibenge. 

Mwinyi Zahera, aliyewahi kufanya kazi kwa karibu na Ibenge wakati wakiinoa timu ya taifa la DR Congo, ametoa ushauri kwa Wananchi kuelekea mchezo huo ambao utachezwa Jumanne ya Novemba 26 Uwanja wa Benjamini Mkapa, akitoa tahadhari na mbinu za kukabiliana na Al-Hilal.

Zahera, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa ufundi wa Namungo amewaambia Yanga kuwa makini sana katika kujenga mashambulizi yao.

Alisisitiza kuwa, kama watashindwa kuwa makini, wanaweza kukutana na mashambulizi ya kushtukiza kutoka kwa Al-Hilal, kama ilivyotokea kwenye mchezo wa mwisho baina ya timu hizo.

“Yanga wanahitaji kuzingatia zaidi katika kujilinda na kutokubali mashambulizi ya haraka ya Al-Hilal. Hawa ni mabingwa wa Sudan, na mara nyingi wanapocheza nje ya uwanja wao wanaweza kuwa hatari sana katika mashambulizi ya kustukiza,” alisema Zahera.

Yanga na Al-Hilal walikutana kwa mara ya mwisho Oktoba 8, 2022, katika mchezo wa raundi ya pili wa kuwania nafasi ya kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa. Katika mchezo huo, walitoka sare ya 1-1 jijini Dar es Salaam, lakini Yanga ilitupwa nje baada ya kupoteza ugenini mchezo wa marudiano kwa bao 1-0. Mchezo huo uliwaacha Wananchi na maumivu, lakini pia somo muhimu kuhusu jinsi ya kukabiliana na timu ngumu kama Al-Hilal.

“Ibenge ni mtaalamu wa kutumia mbinu za kushtukiza na kubadilika haraka. Yanga wanahitaji kuwa na nidhamu na kuzingatia katika dakika zote za mchezo. Hii itawasaidia kuepuka mashambulizi ya ghafla ambayo Al-Hilal wanaweza kutumia wakati wowote,” alisisitiza Zahera.

Zahera aliwataka Yanga kucheza kwa nidhamu na kutokubali kupoteza mpira kirahisi katika maeneo ya hatari.

Related Posts