AKILI ZA KIJIWENI: Asante Simon Msuva, Taifa halikudai

TUMEKUBALIANA kwa pamoja taifa la Tanzania halimdai chochote kwa sasa mshambuliaji wetu nyota, Saimon Msuva kutokana na kile anachokifanya kwenye timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

Jamaa kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita amekuwa mchezaji muhimu na mwenye mchango mkubwa kwa Stars na kiukweli ambaye hakubali kile anachokifanya basi atakuwa na chuki binafsi.

Embu tuangalie baadhi ya mambo ambayo Msuva ameyafanya kwa Stars kisha anayeona staa wetu huyu tunampa sifa za bure ajitathmini mwenyewe kama anamtendea haki au la.

Kwa sasa, Msuva anashika nafasi ya pili katika chati ya wafungaji bora wa muda wote wa Stars akiwa amepachika mabao 24 huku akizidiwa bao moja na Mrisho Ngasa (25).

Tulipofuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon), Msuva alipachika mabao mawili kati ya sita ambayo Stars ilifunga katika mechi sita za kuwania kufuzu.

Katika harakati za kuwania kufuzu fainali za Afcon 2023 ambazo Tanzania baadaye ilikata tiketi ya kushiriki, Stars ilifunga mabao matano katika mechi zote sita za kundi lake na kati ya hayo, mawili yalikuwa ya Msuva.

Safari hii, mwamba kafunga mabao mawili kati ya matano ambayo Tanzania tumeyapata katika kundi letu H la kuisaka tiketi ya kwenda kule Morocco mwakani kwenye Afcon.

Kiukweli Msuva anaipambania sana timu ya taifa na juhudi zake hizo zimekuwa na matunda chanya kwa timu kama kumbukumbu zinavyoonyesha jinsi alivyotubeba mara tofauti katika kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika.

Wasiwasi wetu kijiweni ni kibaba hii sasa umri wake unaelekea ukingoni na muda utafika atalazimika kujiweka kando ili kupisha wadogo zake waendeleze kijiti alichokishika kwa sasa.

Hao wadogo zake shida hawatupi matumaini mwamba wanaweza kuvaa viatu vyake na kufanya kama alivyofanya yeye au zaidi ya hapo kwa sababu wanakosa muendelezo wa kufanya vizuri kuanzia katika klabu zao hadi timu ya taifa.

Related Posts