Rio De Janeiro. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema licha ya utajiri uliopo duniani ila bado kuna changamoto ya umasikini, njaa, magonjwa, utapiamlo na uzalishaji duni barani Afrika.
Amesema idadi kubwa ya watu hususani vijana wanakumbana na changamoto zinazozidi kuwa mbaya kutokana na mizozo na sera za kimataifa zinazoongeza uhaba wa chakula, kukandamiza ushindani na kupunguza upatikanaji wa masoko na teknolojia muhimu.
Ameyasema hayo katika kikao cha viongozi wa nchi wanachama wa G20 juu ya mapambano dhidi ya njaa na umaskini, huko Rio De Janeiro chini Brazil alipoalikwa kuhudhuria mkutano huo na Rais wa Lula da Silva, Novemba 18 na 19, 2024.
Watu wengi bado wanangojea ahadi ya utandawazi kutimizwa, huku wakiwa na matumaini kwamba mageuzi katika utawala wa kimataifa yataleta uwakilishi wa haki na upatikanaji wa rasilimali zinazohitajika kutokomeza umaskini.
“Tunaamini dunia yenye haki, ustawi na endelevu itapatikana pale ambapo nchi zinazoendelea kama yangu zitapata msaada, rasilimali, na uwakilishi unaohitajika kuhamasisha maendeleo endelevu.
“Hata hivyo, ikiwa dunia itabaki kama ilivyo, swali tutakalouliza mwaka 2030 halitakuwa tulishindwa vipi kufikia malengo ya SDGs, bali ni wangapi wengine wameachwa nyuma na dunia,” amehoji.
Ameongeza licha ya vikwazo tulivyokumbana navyo, Tanzania imefanikiwa kutekeleza mageuzi ya kisera na kimfumo, sambamba na uwekezaji wa kimkakati kubadilisha mifumo ya kilimo na chakula.
Amesema kwa kuwa asilimia 61.5 ya Watanzania wanajihusisha na kilimo, juhudi zimeongeza kiwango cha ukuaji wa sekta hii kuwa asilimia 4.2 zimefikia kiwango cha kujitosheleza chakula kwa asilimia 128, na kupunguza kiwango cha umaskini hadi asilimia 26.4 mwaka 2023.
“Hata hivyo, changamoto bado zipo, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mitambo, mbolea, utafiti na maendeleo. Tunaamini kuwa kwa msaada, tunaweza kutumia vyema ubunifu, kujenga ustahimilivu, na kuhamasisha ukuaji unaoshirikisha kila mtu,” amesema.
Rais Samia ameiomba G20 kwanza uhamasishaji wa Haki ya Maendeleo (SDRs) kwa Taasisi za Fedha za Afrika kama vile Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Aidha ameomba mahitaji ya mfumo wa haki zaidi wa uratibu katika mfumo wa kifedha wa kimataifa ulipo sasa.
Pia amesema Tanzania inatoa wito wa kuongeza mifumo ya msamaha wa madeni, misaada na mikopo ya masharti nafuu ambayo itajibu mahitaji ya nchi; “Pia, tunaunga mkono ushirikiano wa nguvu kama vile Muungano wa Kimataifa wa G20 dhidi ya Njaa na Umaskini ili kuhamasisha ubunifu na ukuaji unaoshirikisha watu wote.”
Amesema mkutano huo unadhihirisha dhamira ya pamoja ya kutoacha dunia kama ilivyo. Lazima tuongeze juhudi zetu, na kuhamasisha ahadi zetu za kujenga dunia yenye haki, ustawi na haki kwa wote.
Tanzania ilipata mwaliko huku Rais Samia akiwa mkuu wa nchi wa kwanza kushiriki mkutano wa nchi hizo za G20 zinazochangia asilimia 85 ya pato la jumla la dunia na asilimia 75 ya biashara ya kimataifa.
Hata hivyo awali, Rais wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa na wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete waliwahi kushiriki mikutano ya aina hiyo wakati umoja huo ukiitwa G8, kabla ya mabadiliko ya mwaka 2008.
G20 inajumuisha nchi za Argentina, Australia, Brazil, Canada, China, Ufaransa, Ujerumani, India, Indonesia, Italia, Japani, Jamhuri ya Korea, Mexico, Urusi, Saudi Arabia, Afrika Kusini, Uturuki, Uingereza na Marekani, kadhalika mashirika mawili ya kikanda, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika.