Bei ya tangawizi yapaa Moshi ikifikia kilo Sh7000, ukame watajwa

Moshi/Dar. Watumiaji na walaji wa tangawizi Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro wamelalamikia kupanda bei ya bidhaa hiyo kutoka Sh2,000 hadi Sh7,000 kwa kilo moja, huku hali hiyo ikitajwa kusababishwa na ukame.

Hali hiyo imewalazimu wafanyabiashara wa mkoa huo, kuagiza bidhaa hiyo nchini Ethiopia ili kukidhi mahitaji ya watumiaji.

Mwananchi limepita katika masoko mbalimbali ya Manispaa hiyo ikiwemo soko la Manyema na Mbuyuni na kushuhudia wafanyabiashara hao wakiuza bidhaa hiyo kati ya Sh 6000 hadi Sh 7000 kwa kilo moja.

Zao hilo linalimwa kwa wingi hapa nchini huku mkoa wa Kilimanjaro ukitajwa kulima zao hilo kwa zaidi ya asilimia 70 ya uzalishaji wake, ambapo kwa mwaka zao hilo huzalisha tani 15,400 kati ya tani 22,000 zinazozalishwa hapa nchini kwa mwaka.

Wakizungumza na Mwananchi digital leo, wakulima wa tangawizi Wilaya ya Same, wamesema ukame ulioikumba wilaya hiyo kwa miaka mitatu mfululizo, umeathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa zao hilo tofauti na vipindi vilivyopita.

John Gosso ambaye ni mkulima wa tangawizi wilayani Same, amesema kuadimika kwa bidhaa hiyo kunatokana na uchache wa mvua na kwamba zao hilo linahitaji mvua ya kutosha.

“Mvua zimekuwa adimu mno na tangawizi inahitaji mvua nyingi, mpaka sasa hali sio nzuri, mwaka jana kilo moja ya tangawizi ilikuwa Sh2,000 na gunia ilikuwa ni Sh200,000 ila kwa sasa bei yake haishikiki,” amesema Gosso.

Wilison Mjema, mkulima wa kijiji cha Pinchi, Same, amesema licha ya kwamba kilimo cha tangawizi ndicho kinachotegemewa na wananchi wa wilaya hiyo, misimu mitatu iliyopita walishindwa kuvuna kutoka na ukame uliosababisha zao hilo kukauka mashambani.

“Kukauka kwa tangawizi kutokana na ukame kumetupa wakati mgumu sana, maana hili zao ndio tunalolitegemea kutusomeshea watoto pamoja na kutupatia fedha kwa ajili ya kuendeleza shughuli nyingine za kiuchumi.

Lakini ukame uliotokea kwa vipindi mfululizo umetuangusha hatuna chochote, ndio tunasubiria msimu unaoanza tuone itakuwaje,” amesema Mjema.

Watumiaji wa tangawizi walalama

Wakizungumzia kuadimika kwa bidhaa hiyo, wananchi hao, wamesema hapo awali walikuwa wakinunua bidhaa hiyo kuanzia Sh500,  lakini kwa sasa kipimo hicho hakuna na kwamba wanalazimika kununua kuanzia Sh1,000 na kuendelea hali ambayo wamesema inawagharimu.

Anaulirka Ngowi, mkazi wa Moshi, amesema kuadimika kwa bidhaa hiyo sokoni wanalazimika kunywa chai ambayo haina kiungo cha tangawizi kama walivyozoea kutokana na bei kuwa kubwa.

“Sasahivi ukienda sokoni hupati tangawizi ya Sh500 na ndio tulikuwa tumezoea kununua hivyo, kwa hiyo ukitaka tangawizi ni kuanzia Sh1,000 kitu ambacho hatujawahi kuona, miaka yote tumekuwa tukinunua kwa Sh 500 lakini Sasa imekuwa ni ngumu na ni wafanyabiashara wachache ndio wanaouza bidhaa hiyo,” amesema Anaulirka na kuongeza:

“Watu ambao ni wa kipato cha chini tunashindwa kumudu hii bei, kununua tangawizi Sh1000 ni mtihani, wakati mwingine tunakunywa chai ambayo haina tangawizi.”

Eneka James, mkazi wa Kiboriloni amesema kupanda bei kwa bidhaa hiyo kunawafanya washindwe kutumia bidhaa hiyo kwenye chakula.

“Tushazoea kuweka tangawizi kwenye nyama lakini kutokana na bei kuwa juu tunashindwa kununua kwa sababu ukinunua tangawizi ya Sh1,000 haitoshi ni ndogo sana kulingana na mahitaji ya familia, na ukitaka tangawizi ya kutosha familia nzima ni gharama,” amesema Eneka

Walichokisema wafanyabiashara

John Kanje, mfanyabiashara wa soko hilo, amesema wanalazimika kuuza bidhaa hiyo kwa bei kubwa kutokana na kuadimima kwa bidhaa hiyo na kwamba iliyopo ni tangawizi kutoka nchini Ethiopia na uingizwaji wake ni gharama.

“Sasa hivi tangawizi hakuna kabisa, tangawizi iliyopo ambayo ndio hii tunayouza inatoka nchi ya Ethiopia, kilo moja tunanunua Sh5000 hivyo na sisi tunalazimika kuuza kilo moja Sh6000 hadi Sh7000,” amesema Kanje.

Mfanyabiashara mwingine, Agness Tesha amesema: “Ni kipindi kigumu sana kwetu wafanyabiashara wadogo, sasa hivi wanaouza tangawizi ni matajiri wakubwa ambao walinunua mzigo mkubwa ndio sasa wanauza kilo moja ni Sh 7000 wakati mwaka jana kilo moja ya tangawizi ilikuwa Sh1500 hadi Sh2000,”

Akizungumzia changamoto hiyo, Ofisa kilimo mkoa wa Kilimanjaro, Godwin Maro  amesema kuadimika kwa bidhaa hiyo, kunatokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha ukame kwa vipindi vitatu mfululizo hivyo kuathirii uzalishaji wa zao hilo.

“Pamekuwa na ukame kwa muda mrefu kwenye maeneo mengi, na hii imesababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi, zao la tangawizi ni moja ya zao linalohitaji maji mengi, hivyo kukosekana kwa mvua kumeathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji wake,”amesema Maro

Kuhusu bidhaa hiyo kuagizwa nje ya nchi amesema ni fursa kwa wafanyabiashara kutafuta bidhaa hiyo maeneo mengine ili kukidhi mahitaji ya walaji.

“Kama bidhaa ikikosekana ni fursa kwa wafanyabiashara kutafuta sehemu wanayoweza kupata kwa sababu wateja wapo na ni bidhaa inayohitajika,” amesema Maro

Pamoja na mambo mengine, amewataka wananchi kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti ya kutosha ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Mfanyabiashara wa jumla katika soko la Mabibo jijini Dar es Salaam, Nicholous Julius, amesema tangawizi katika soko hilo kwa sasa gunia ni Sh450,000 kutoka Sh130,000 hadi Sh150,000 waliokuwa wananunua awali.

Wakati kilo iliyokuwa ikiuzwa kati ya Sh1300 hadi Sh1500 hivi sasa kwa bei ya jumla inauzwa kati ya Sh4,000 hadi Sh4,500.

Elitumaini Tumaini, mfanyabiashara wa tangawizi soko la Ilala, amesema tangawizi inayopatikana kwa sasa ni ya Ethiopia ambayo bei yake kwa kilo ni Sh3,200 kwa bei ya jumla huku gunia likiuzwa Sh320,000.

Wakati ile ya Moshi Same amesema inauzwa kati ya Sh4300 hadi Sh4500 kwa kilo bei ambayo haijatofautiana sana na inayotoka Morogoro.

Elly Amani, mmiliki wa Genge Chanika amesema kutokana na kupanda kwa bidhaa hiyo, hivi sasa tangawizi aliyokuwa anaiuza Sh200 anauza Sh500 huku lile fungu alilokuwa akiuza Sh500 analiuza Sh1000.

Nora Kimasha mkazi wa Buza na Mfanyabiashara wa genge, amesema kilo ya tangawizi kwa sasa anauza kati ya Sh6000 hadi Sh6500 kutoka Sh3000 hadi Sh4000 aliyokuwa akiuza mwanzo.

“Hesabu hizi zinakuja kwa kuwa kuna gharama hapo umeitumia kuitoa sokoni hadi kuifikisha huku kwa mteja wa juu hivyo lazma uzifidie kurudisha hela yako,”amesema Nora.

Related Posts