Dk Jafo: Wahitimu changamkieni soko huru Afrika

Dodoma. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amewataka wahitimu wa vyuo vikuu nchini kutumia elimu na ujuzi walioupata kujiajiri na kuchangamkia fursa katika soko huru la Afrika.

Dk Jafo ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Novemba 21, 2024 kwenye mahafali ya 59 ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kampasi ya Dodoma alipokuwa mgeni rasmi.

Akizungumzia suala la ajira, Waziri Jafo amesema kutokana na uwingi wa wahitimu wa chuo kila mwaka, Serikali haiwezi kuajiri wote, hivyo hawana budi kutumia ujuzi vyema.

“Itumieni elimu ya biashara mliyoipata kwenye fursa mbalimbali zilizopo nchini kwa kuhakikisha mnakamata kila fursa inayojitokeza mbele yako ilimradi tu iwe halali,” amesema Dk Jafo

Pia, amewataka wahitimu hao kuwa waaminifu kwenye shughuli zao ili waweze kuamika na jamii badala ya kutumia ujanja ujanja kwenye biashara zao.

“Itumieni elimu ya biashara mliyoipata kwenye fursa mbalimbali zilizopo nchini kama vile kwenye reli ya mwendokasi (SGR) ambayo itaanza kusafirisha mizigo kwenye nchi ambazo hazina bandari.

“Lakini pia kwenye michuano ya Afcon (Michuano ya Mataifa ya Afrika—Mpira wa miguu) ambayo inakusanya watu wengi kwa wakati Moja,” amesema Dk Jafo.

Awali, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Edda Lwoga, alisema katika kuhakikisha wanaboresha elimu wanayoitoa, tafiti na ushauri wa kitaalamu wanashirikiana na mashirika tofauti ya ndani na nje ya nchi.

“kwa kushirikiana na mashirika haya yote tumefanikiwa katika kuwezesha wanachuo wetu na wahadhiri kupata elimu ya Daktari wa Falsafa na Shahada ya uzamili lakini pia kutengeneza mitalaa ambayo tutaanza kuitumia mwaka 2025,” amesema Profesa Lwoga

Related Posts