The Hague. Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) wametoa hati ya kuwakamata Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, waziri wa zamani wa ulinzi, na kamanda wa kijeshi wa wanamgambo wa Hamas.
Kwa mujibu wa hati hiyo iliyotolewa leo Alhamisi, Novemba 21, 2024, wengine wanaotakiwa kukamatwa ni waziri wa zamani wa ulinzi wa Israel, Yoav Gallant na Kamanda wa Hamas, Mohammed Deif, ingawa Jeshi la Israeli limesema aliuawa katika shambulio la anga huko Gaza Julai mwaka huu.
Mei 2024, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Karim Khan aliomba vibali kwa majaji wa mahakama hiyo vya kuwakamata Netanyahu, Gallant, Deif na viongozi wengine wawili wa Hamas ambao wameuawa tangu wakati huo, Ismail Haniyeh na Yahya Sinwar.
Ingawa Israel inaamini kuwa Deif amekufa, mahakama hiyo ilisema iliarifiwa na Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC kwamba haikuwa katika uwezo wa kuamua iwapo aliuawa au bado yupo hai.
Tuhuma zinazowakabili ni madai ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu wakati wa vita kati ya Israel na Hamas. Israel na Hamas wamekataa madai hayo.
Kwa mujibu wa ICC, kesi ya mwendesha mashtaka dhidi ya watuhimiwa hao inatokana na shambulio la wapiganaji wa Hamas la Oktoba 7, 2023, lililofanywa kusini mwa Israel na kuua takriban watu 1,200 na wengine zaidi ya 251 kutekwa mateka huko Gaza.
Israel inatuhumiwa kwa kujibu mashambulizi kwa kuanzisha kampeni ya kijeshi ya kuwaondoa Hamas, ambapo takriban watu 44,000 wameuawa huko Gaza, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.
Mahakama yenyewe haina polisi wa kutekeleza vibali, badala yake inategemea ushirikiano kutoka kwa nchi wanachama wake.
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kutagemea ushirikiano wa nchi 124 wanachama wa ICC, ambapo Israel na washirika wake kama Marekani siyo wanachama wa ICC.
Rais wa Israel, Isaac Herzog alisema: “Ikichukuliwa kwa nia mbaya, uamuzi wa kikatili katika ICC umegeuza haki ya wote kuwa kicheko cha ulimwengu.”
“Uamuzi huo umechagua upande wa ugaidi na uovu badala ya demokrasia na uhuru, na kugeuza mfumo wenyewe wa haki kuwa ngao ya binadamu kwa uhalifu wa Hamas dhidi ya ubinadamu,” alisema Herzog.
Mustafa Barghouti, mwanasiasa mkongwe wa Palestina anayeishi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Isarel, amefurahia waranti ya kukamatwa Netanyahu na Gallant.
“Pia tunatoa wito kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuharakisha uamuzi wake juu ya Israel kufanya uhalifu wa mauaji ya halaiki,” alisema.
Septemba mwaka huu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ilisema iliwasilisha hoja mbili za kisheria kupinga mamlaka ya ICC na kusema kuwa mahakama hiyo haikuipa Israel fursa ya kuchunguza madai yenyewe kabla ya kuomba hati hizo.
“Hakuna demokrasia nyingine iliyo na mfumo huru na unaoheshimika wa kisheria kama ule uliopo nchini Israeli ambao umetendewa kwa njia hii ya chuki na mwendesha mashtaka,” Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Oren Marmorstein aliandika kwenye X.
Alisema Israel imebaki ‘imara katika kujilinda kwake kwa utawala wa sheria na haki’ na itaendelea kuwalinda raia wake dhidi ya wanamgambo.
Awali, ICC ilisema inatafuta kibali cha kukamatwa kwa Ismail Haniyeh, kiongozi wa Hamas ambaye aliuawa katika mlipuko mjini Tehran nchini Iran Julai mwaka huu.
Pia, iliondoa ombi lake la kutaka kibali dhidi ya Yahya Sinwar, msanifu mkuu wa mauaji ya Oktoba 7 na mrithi wa Haniyeh, baada ya kuuawa na majeshi ya Israel huko Gaza mwezi uliopita.
Machi 17, 2023 ICC ilitoa hati ya kukamatwa Rais Vladimir Putin wa Urusi akitumiwa kwa mauaji ya kivita nchini Ukraine.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.