Taarifa ya Mahakama ya ICC imesema majaji wa mahakama hiyo wametoa hati za kukamatwa kwa watu wawili, Benyamin Netanyahu na Yoav Gallant. Viongozi hao wanatuhumiwa na mahakama hiyo ya kimataifa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita uliofanywa angalau kuanzia Oktoba 8, 2023 hadi Mei 20, mwaka huu.
Mei 20 ndio tarehe ambayo mwendesha mashtaka wa ICC, Karim Khan aliwasilisha maombi hayo ya kutolewa hati za kukamatwa kwa viongozi wa Israel. Mahakama ya ICC imeongeza katika taarifa nyingine kwamba hati ya kukamatwa pia ilitolewa dhidi ya Mohammed Deif, mkuu wa tawi la kijeshi la Hamas.
Shutuma hizi zinahusu mashambulizi mabaya ya Israel kufuatia shambulizi liliyofanywa na Hamas tarehe 7 Oktoba mwaka jana. Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu ICC inasema ina “misingi ya kuridhisha ya kuamini” kwamba Netanyahu na Gallant wanawajibika kwa uhalifu wa kivita wa kutumia njaa kama njia ya vita, uhalifu dhidi ya ubinadamu ikiwa ni pamoja na mauaji, mateso na vitendo vingine vya kikatili na mashambulizi yaliyoelekezwa kwa makusudi dhidi ya raia.
Kuhusu Mohammed Deif, anayetuhumiwa kuwa mpangaji mkuu wa shambulio la Oktoba 7 nchini Israel na ambaye kulingana na Israeli aliuawa mnamo Julai 13, mahakama ya ICC, imesema ikizingatia “kutokuwa na uthibitisho wa kifo chake”, iliamua pia kutoa hati ya kukamatwa kwake.Mwendesha mashtaka Mkuu wa Mahakama ya ICC anatafuta waranti wa kukamatwa viongozi wa Israel na Hamas
Majaji wa ICC wamesema hati hizo za kukamatwa ziliainishwa kama siri ili kulinda mashahidi na kuhakikisha upelelezi unaendelea. Lakini wameweka wazi taarifa hiyo kwa manufaa ya waathiriwa na familia zao kufahamu uwepo wa hati hizo.
Israel haikusita kukosoa vikali hati hizo za kukamatwa kwa Netanyahu na Gallant. Taarifa ya ofisi ya Waziri mkuu wa Isreal imeiita hatua ya mahakama ya ICC kuwa kitendo cha chuki dhidi ya Wayahudi. Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa Israel inakataa kwa kuchukizwa na vitendo vya kipuuzi na vya uwongo vya mahakama ya ICC dhidi yake.Pretoria yakaribisha ombi la ICC la kutaka kukamatwa kwa viongozi wa Israel na Hamas
Pia mahakama hiyo imetoa waranti wa kukamatwa kwa kiongozi wa kijeshi wa kundi la Hamas, Mohammed Deif, anayejulikana pia kwa majina ya Ibrahim Al-Masri.
Kundi la Hamas limepongeza hatua ya mahakama ya ICC na kuiita kama ‘hatua muhimu kuelekea haki’. Serikali ya Jordan imesema lazima hatua hiyo ya ICC lazima iheshimike na itekelezwe. Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema hati za kukamatwa za ICC sio za kisiasa na uamuzi wa mahakama unapaswa kuheshimiwa na kutekelezwa.
“Kama nilivyosema hapo awali, mkasa wa Gaza lazima ukome. Na sasa nitakuwa na akili timamu katika maoni yangu. Sio uamuzi wa kisiasa, ni uamuzi wa mahakama, mahakama ya haki, mahakama ya kimataifa. Na uamuzi wa mahakama unapaswa kuheshimiwa na kutekelezwa kwa hiyo ninazingatia uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kutoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu Netanyahu, Waziri wa Ulinzi wa zamani Gallant na viongozi wa Hamas ni uamuzi wa lazima kwa mataifa yote, nchi zote wanachama wa ICC, ambazo zinajumuisha wanachama wote wa Umoja wa Ulaya, zinawajibika kutekeleza uamuzi huu wa mahakama.”
Kwa upande wake wake Ufaransa imesema itaheshimu maamuzi ya mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.Uamuzi wa Afrika kusini kuipeleka Israel ICC- waibua mjadala
Hata hivyo, Israel iliendelea na mashambulizi yake ya angani hii leo huko kusini mwa mji wa Beirut, nchini Lebanon. Na kwa mujibu wa Wizara ya Afya inayoendeshwa na kundi la Hamas huko Gaza, takriban watu 71 wameuawa katika muda wa saa 24 zilizopita kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel.