Kulikobaki ni CCM tu, wananchi pigeni kura ya hapana

 

KIONGOZI mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amezungumza kwa msisitizo kuhusu mapambano ya chama hicho kuhakikisha uchaguzi wa serikali za mitaa unafanyika kwa haki, huku akiwataka wananchi wa kijiji cha Ilalanguru, Jimbo la Kigoma Kusini, mkoani Kigoma kuchagua viongozi wanaowajibika. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kigoma … (endelea).

Akihutubia wananchi hao tarehe 21 Novemba 2024, Zitto amebainisha hatua zilizochukuliwa na ACT Wazalendo kudai haki ya demokrasia.

“Miaka mitano iliyopita, uchaguzi kama huu tunaoifanya ulivurugwa, watu wakapitishwa bila kupingwa, wakatangazwa kuongoza vijiji na mitaa yetu bila ridhaa yenu. Mwaka huu figisu zipo, watu wameenguliwa lakini hakuna aliyetangazwa kupita bila kupingwa kwasababu chama chenu cha ACT Wazalendo kilichukua hatua muhimu sana, kiliishitaki serikali kwa mambo hayo ya kupita bila kupingwa, tukaiambia mahakama kwamba serikali inatekeleza sheria ya kupitisha watu bila kupingwa lakini hiyo sheria ni kinyume cha katiba, tukashinda,” amesema Zitto.

Akielezea mikakati ya ACT Wazalendo kupitia ilani yao ya uchaguzi ambayo ni maalumu kwa serikali za mitaa, Zitto ameahidi kuwa chama hicho kitarejesha uwazi na uwajibikaji katika ngazi ya vijiji. Ameeleza kuwa viongozi watakaochaguliwa kupitia chama hicho watahakikisha wanarudisha sauti za wananchi kwa kufuata maelekezo ya ilani ya uchaguzi.

“Mtakapogawiwa ilani yetu hii, chama chetu kimetoa ilani ya uchaguzi wa serikali za mitaa, tumeeleza tutafanya nini. Moja ya ahadi ambayo tumewapa kwenye ilani yetu ni kwamba viongozi wetu watakaochaguliwa, watafanya mikutano mikuu ya kijiji. Tutawarudishia sauti za vijiji vyenu, tutarudisha sauti ya Kijiji chenu cha Ilalanguru kwenu. Kila miezi mitatu lazima kuwe na mkutano mkuu wa kijiji, kwani kwa miaka mitano iliyopita utawala uliokuwepo haukuweka mkutano hata mmoja, mkutano ambao mtajadili mambo yenu,” ameeleza Zitto.

Aidha, Zitto amesisitiza kuwa uwajibikaji ni msingi wa chama cha ACT Wazalendo. Alisema, “Haya ndiyo maelekezo ya ilani. Mwenyekiti anayetokana na ACT Wazalendo asipofanya hivyo mara tatu mfululizo, tunamfukuza uanachama tunakuja kuwaambia tupeni mtu mwingine wa kuweza kufanya hivyo.”

Kiongozi huyo mstaafu amesisitiza zaidi umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024, na kuchagua viongozi wanaoonesha dhamira ya kweli ya kuwajibika kwa maslahi ya jamii.

About The Author

Related Posts