Ladies First kuanza kesho | Mwanaspoti

MASHINDANO ya riadha ya wanawake (Ladies First) msimu wa sita yanatarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia kesho Ijumaa hadi keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, alisema mashindano hayo yatashirikisha wanariadha 155 na viongozi kutoka mikoa 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar

Alisema pia wataendesha semina kuhusu masuala ya wanawake pamoja na mafunzo kwa makocha.

“Katika ufunguzi tunatarajia mgeni rasmi kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Damas Ndumbaro,” alisema Msitha.

Aliongeza kuwa hafla ya ufunguzi itaambatana na matukio mbalimbali yakiwamo mazoezi ya viungo na jogging ikihusisha vikundi 500 kutoka Temeke.

“Msimu huu utakuwa tofauti, awali ilikuwa ikishirikisha umri tofauti na sasa kutakuwa na vigezo kwa washiriki, walengwa ni wasichana chini ya umri wa miaka 20 tukiwa na lengo la kuibua vipaji vipya,” alisema.

Alisema washiriki watashindana katika mbio za mita 100, 200, 400, 800, 1500, 5000, 10000, 4×100 kupokezana vijiti na kurusha mkuki.

Naye mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan, Ara Hitoshi, alisema lengo ni kuimarisha ushiriki wa wanawake katika michezo.

Alisema kuwa mashindano hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kutoa fursa kwa wanawake na wasichana na kuchochea usawa wa kijinsia katika michezo.

Balozi wa JICA, Juma Ikangaa, alitoa wito kwa wazazi kuwapa nafasi watoto waweze kushiriki ili kujenga usawa katika michezo.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Felix Chunga, alisema watasimamia kiufundi na kuzingatia umri ili kupata vipaji vipya vitakavyokuwa nembo ya taifa hapo baadaye.

Related Posts