Dar es Salaam. Wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) likiitaja Tanzania kuongoza ukanda wa Afrika Mashariki katika kukabiliana na magonjwa ya dharura na majanga, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maelekezo akitaka kuimarishwa mfumo wa udhibiti changamoto hizo zinapojitokeza.
Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, Dk Matshidiso Moeti leo Novemba 21, 2024 ameitaja Tanzania kama nchi inayofanya vizuri katika kukabiliana na magonjwa ya dharura, akitoa mfano wa mlipuko wa Uviko-19 na Maburg namna ulivyodhibitiwa.
“Tumeshuhudia namna Tanzania inavyofanya vizuri ukanda wa Afrika Mashariki katika kukabiliana na hali ya dharura licha ya uwepo wa changamoto ndogo-ndogo ambazo zinaweza kufanyiwa kazi, ikiwemo uchache na uimara wa rasilimaliwatu,” amesema.
Akizungumza kwenye mkutano wa pamoja wa mawaziri na viongozi wa juu wa WHO kuhusu hali ya utekelezaji wa afya kwa wote na utayari wa kukabiliana na dharura na majanga, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kuchukua hatua kukabiliana na magonjwa na majanga.
Miongoni mwa maelekezo aliyotoa Majaliwa ni kuzitaka taasisi na idara zinazojihusisha na sekta ya afya, kuchukua tahadhari kwa kufanya tathmini ya viashiria vya majanga na magonjwa ya mlipuko, ili kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa kwa wakati.
Maelekezo mengine ni wizara, idara na taasisi za mamlaka za serikali za mitaa kuandaa mikakati mahususi ya kukabiliana na dharura hizo, ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti kutekeleza shughuli za kipaumbele zinapotokea changamoto za magonjwa ya mlipuko na majanga.
“Niitake pia Wizara ya Afya isimamie uwekezaji katika kuimarisha taasisi za utafiti ili ziwe na uwezo mkubwa wa kutambua vimelea vya magonjwa ya mlipuko na kuhakikisha vituo vyote vya afya vina uwezo wa kushughulia dharura zinapotokea,” amesema na kuongeza:
“Kingine muhimu ninachota kifanyiwe kazi ni kuwezesha umma kuwa na uelewa mkubwa wa majanga na magonjwa ya dharura. Tunaweza kuwa na mifumo mizuri ndani ya Serikali lakini kupata matokeo chanya ni lazima elimu hiyo ishuke kwa wananchi.”
Mkuu wa Kitengo cha Dharura WHO, Dk Erasto Silvanus amesema tathimini inaonyesha licha ya mafanikio katika eneo hilo, Tanzania inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo upungufu wa rasilimali watu kwa ajili ya afya katika ngazi zote kwenye sekta ya umma na binafsi.
Ametaja changamoto nyingine ni kutokuwepo mpango wa kitaifa wenye kutoa mwongozo wa namna ya kupokea rasilimali watu wakati wa dharura za afya na ukosefu wa mwongozo wa taifa wa huduma endelevu za afya wakati wa dharura.
Nyingine ni upungufu wa timu za matibabu ya dharura kwa ajili ya kupelekwa kwa haraka wakati wa dharura za afya ya jamii.
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amesema wizara imeendelea kufuatilia maelekezo ya WHO na hasa katika kusimamia nguzo zinazojenga umuhimu wa sekta ya afya.
“Kazi yetu ni kuhakikisha Watanzania wanakuwa salama dhidi ya magonjwa ya mlipuko na majanga. Tumepata majanga kadhaa ikiwemo Maburg, maporomoko ya udongo Hanang, mafuriko na hili la Kariakoo lakini tumefanya kazi kwa kushirikiana kukabiliana nayo.
“Tunasimamia mifumo inayosimamia sekta ya afya kuhakikisha inakwenda mbele. Tunataka kuhakikisha mifumo yote inasomana kufikia Desemba kama ambavyo imeelekezwa na kiongozi mkuu wa nchi,” amesema.
Mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa Azimio la Mkutano wa 73 wa Afya Duniani uliofanyika mwaka 2020 kuhusu utekelezaji kwa hiari wa mapitio shirikishi ya hali ya utekelezaji wa afya kwa wote na utayari dhidi ya dharura za kiafya kwa nchi wanachama wa WHO.