Mama kizimbani akidaiwa kumnyonga mtoto wake wa siku moja

Dar es Salaam. Amina Ally (21), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kwa kesi ya jinai kujibu shtaka la kumuua mtoto wake mchanga mwenye umri wa siku moja.

Amina, mkulima na mkazi wa Kigogo wilayani Kinondoni, Dar es Salaam alipandishwa kizimbani jioni ya jana Novemba 20, 2024 alikosomewa shtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Saada Mohamed.

Anadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 27, 2024 eneo la Kigogo, Manispaa ya Kinondoni kinyume cha kifungu cha 199 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, kama ilivyorejewa mwaka 2022.

Kifungu hicho kinasema: “Pale mwanamke kwa kitendo chochote cha makusudi au kuacha kutenda kitendo hicho amesababisha kifo cha mtoto wake mwenye umri wa chini ya miezi 12, lakini wakati wa kitendo hicho mama huyo alikuwa hajapona kutokana na kuzaa mtoto huyo na kwa sababu hiyo au kwa sababu inayohusiana na unyonyeshaji baada ya kuzaa mtoto huyo akili yake ilidhurika, bila kujali kwamba mazingira yalikuwa hivyo lakini kwa kufuata kifungu hiki ingaliweza kuwa kosa la kuua kwa kukusudia, atakuwa na hatia ya kosa la kuua mtoto mchanga, na anaweza, kushughulikiwa na kuhukumiwa kwa kosa kana kwamba alikuwa na hatia ya kumuua mtoto huyo bila kukusudia.

Upande wa mashtaka umedai siku ya tukio mshtakiwa kwa makusudi alimnyonga mtoto wake mwenye umri wa siku moja na kumsababishia kifo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo Is-haq Kupa anayesikiliza kesi hiyo alimuuliza mwendesha mashtaka iwapo mshtakiwa anaruhusiwa kujibu shtaka hilo.

Hakimu Kupa alimweleza mshtakiwa hatakiwi kujibu shtaka hilo (kukiri au kukana) katika mahakama hiyo kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo bali inapita tu, kwani itasikilizwa na Mahakama Kuu, ambako atakuwa na haki ya kukiri au kukana shtaka.

Wakili Mohamed aliieleza mahakama kulingana na shtaka linalomkabili mshtakiwa, ana haki ya dhamana akaiomba impe masharti.

Hakimu Kupa amesema kwa shtaka hilo mshtakiwa atatakiwa kuwa na mdhamini mmoja ambaye ni mtumishi wa Serikali atakayethibitishwa na taasisi anayoifanyia kazi, ambaye atatakiwa kusaini bondi ya Sh10 milioni.

Mshtakiwa hakuweza kutimiza sharti hilo. Hakimu Kupa aliamuru apelekwe mahabusu akimweleza siku yoyote akikamilisha sharti hilo hata kabla ya siku nyingine ya tarehe itakayotolewa amri ya kufikishwa mahakamani kwa ajili kudhaminiwa.

Hakimu Kupa aliahirisha kesi hadi Desemba 5, mwaka huu itakapotajwa.

Related Posts