Dar es Salaam. Marekani imemtambua kiongozi wa upinzani wa Venezuela, Edmundo González kama Rais mteule wa nchi hiyo licha ya Nicolás Maduro kushinda nafasi hiyo katika uchaguzi uliofanyika Julai 28, 2024.
Kufuatia taarifa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken aliyoitoa kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), taifa hilo kubwa kwa uchumi duniani imemtambua González ambaye kwa sasa amekimbilia nchini Hispania.
“Watu wa Venezuela kwa nguvu ya pamoja Julai 28, walimfanya Edmundo González kuwa Rais mteule. Demokrasia inahitaji heshima kwa mapenzi ya wapiga kura,” aliandika Waziri Blinken.
Hii ni mara ya kwanza kwa Marekani kumtaja González kama Rais mteule wa Venezuela, hata hivyo hatua hiyo inakuja miezi miwili kabla ya kipindi kipya cha Rais Maduro kuanza rasmi.
Kwa mujibu wa tovuti ya El Pais, Gonzalez ameshukuru kutambuliwa kupitia mtandao wa kijamii ikiwa ni dakika chache baada ya ujumbe wa Blinken,“hatua hii inaheshimu hamu ya mabadiliko ya watu wetu na ishara ya uraia tuliyotekeleza pamoja kwenye uchaguzi,” ameandika kwenye X.
Baraza la Uchaguzi la Kitaifa la Venezuela (CNE) lilimtangaza Maduro kama mshindi, lakini tangu wakati huo halijachapisha matokeo kamili ya kura, licha ya wito kutoka kwa Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi za Amerika ya Latini kama vile Brazil na Colombia.
Hata hivyo, muungano mkuu wa upinzani wa Venezuela, Plataforma Unitaria Democrática (PUD), ulitoa matokeo ya uchaguzi mtandaoni yaliyoonesha González kama mshindi, akiwa na kura zaidi ya mara mbili ya Maduro.
Balozi huyo wa zamani amekuwa uhamishoni nchini Hispania tangu Septemba 2024 alikimbilia huko baada ya kulalamikia mateso kutoka kwa mamlaka za Venezuela.
Ofisi ya mwendesha mashtaka ilifungua uchunguzi dhidi yake na amri ya kumkamata ilikuwa imetolewa baada ya muungano wa PUD kutoa matokeo ya kura mtandaoni.