Mashahidi wawili kutoa ushahidi kesi ya Chuma cha Chuma

Dar es Salaam. Serikali imesema itakuwa na mashahidi wawili wa upande wa mashtaka katika kesi ya jinai inayomkabili raia wa Burundi Ferdnand Ndikuriyo (27) maarufu Chuma cha Chuma.

Chuma anakabilia na shtaka moja la kuwepo nchini bila kuwa na kibali, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Chuma ambaye ni msanii wa muziki na mkazi wa Mbezi Louis, alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 4, 2024 na kusomewa shtaka hilo.

Hata hivyo, leo Alhamisi Novemba 21, 2024, Wakili wa Serikali kutoka Idara ya Uhamiaji, Raphael Mpuya amemsomea maelezo ya awali mshtakiwa hiyo.

Mpuya amemsomea maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga.

Wakili Mpuya alianza kwa kumkumbusha shtaka lake kwa kumsomea na baada ya hapo alimsomea hoja za awali (PH).

Katika maelezo hayo, mshtakiwa huyo anadaiwa kuingia nchini kwa mara ya kwanza, Juni 12, 2022 kupitia mpaka wa Mtukula na alipewa viza ya matembezi ya siku 60 ambayo ilikuwa inaisha muda wake Agosti 11, 2022.

“Baada ya viza kuisha muda wake, mshtakiwa aliendelea kuishi nchini bila kuripoti ofisi za uhamiaji kwa ajili ya kuhuisha taarifa zake,” amedai wakili Mpuya.

Aliendelea kusoma maelezo hayo, Septemba 18, 2024 mshtakiwa alikamatwa na maofisa wa Polisi eneo la Las Vegas Casino, iliyopo Upanga.

Hata hivyo, Oktoba 21, 2024 mshtakiwa alifikishwa ofisi za Uhamiaji Wilaya ya Kinondoni kwa ajili ya hatua za kisheria ikiwemo kufanyiwa mahojiano na kuchukuliwa maelezo ya onyo.

“Katika mahojiano hayo, mshtakiwa alikiri kuwepo nchini kwa sababu viza yake ilikuwa imeisha muda wake,” amedai wakili.

Novemba 4, 2024, mshtakiwa alifikishwa katika mahakama hiyo na kusomewa shtaka linalowakabili.

Mshtakiwa amekubali majina yake, uraia wake, jinsi alivyoingia nchini kupitia mpaka wa Mtukula, huku maelezo mengine akikana kuyatenda.

Kesi hii inaendelea baadaye…

Related Posts