Yanga imeanza mikakati ya kuimarisha safu yake ya ushambuliaji katika dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa Desemba 15 mwaka huu.
Inaripotiwa kuwa mshambuliaji huyo ameshafanya mazungmzo na kumalizana na vigogo wa Yanga ambapo wamefikia pazuri huku kilichobaki kwa mchezaji huyo ni kusubiri dirisha dogo ili ajiunge nayo.
Uwezo wa kufunga na kupiga pasi za mwisho ambao Bayo amekuwa nao unaonekana kuiridhisha Yanga ambayo ujio wa mshambuliaji huyo utasaidia safu yake ya ushambuliaji lakini pia kuwaongezea ushindani chanya washambuliaji waliopo kikosini ambao wanaonekana bado wanajitafuta.
Sifa kubwa ya Bayo ni kufunga mabao ya vichwa akitumia vyema kimo chake cha mita 1.85 (futi 6 inchi 06) lakini pia anasifika kwa mashuti makali anapojongea kwenye lango la timu pinzani.
Kwa sasa, Bayo ni mchezaji huru baada ya kuachana na MFK Vyskov inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Czech ambayo aliichezea mechi 42 na kuifungia mabao manane.
Kabla ya kujiunga na Vyskov, Bayo aliitumikia Ashdod inayoshiriki Ligi Kuu ya Israel ambako katika mechi 41 alizoichezea, alifunga mabao manane huku akipiga pasi moja ya mwisho.
Katika timu ya taifa ya Uganda, mshambuliaji huyo amecheza mechi 21 na kuhusika na mabao tisa, akifunga mabao manane (8) na kupiga pasi moja ya mwisho.
Ni mchezaji mwenye uzoefu kutokana na idadi ya klabu alizowahi kuzichezea ndani ya nje ya Afrika ambazo ni MFK Vyskov (Czech), FC Ashdod (Israel), Bnei Sakhnin (Israel), Buildcon FC (Zambia), Vipers (Uganda) na Proline (Uganda).
“Bayo ni mshambuliaji mzuri na hadi uongozi umefikia hatua ya kuzungumza naye na kumalizana naye, kuna tathmini ya kina ambayo imefanya kabla ya kupitisha jina lake na uzoefu alionao utakuwa msaada kwake kuzoea kwa haraka mazingira ya hapa,” kilifichua chanzo ndani ya Yanga.
Kwa sasa Yanga ina washambuliaji wanne ambao ni Prince Dube, Kennedy Musonda, Clement Mzize na Jean Baleke.
Washambuliaji hao kwa jumla wamefunga mabao manne kati ya 14 yaliyofungwa na timu hiyo katika Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kucheza mechi kumi.
Dube ambaye amecheza mechi tisa kwa dakika 419, hajafunga zaidi ya kutoa asisti moja, huku Mzize akifunga mawili baada ya kucheza mechi zote kumi kwa dakika 457.
Jean Baleke katika mechi nne alizocheza kwa dakika 166, amefunga bao moja, wakati Kennedy Musonda aliyecheza dakika chache zaidi ya wenzake ambazo ni 142 katika mechi saba, amefunga bao moja.