Unguja. Wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini, Unguja llikimshikilia Maulid Hassan Maulid (18) kwa tuhuma za kubaka na kumsababishia kifo mtoto wa miaka sita, mama wa mtoto huyo ameeleza mkasa uliomfika mwanawe.
Mtoto huyo alikuwa anasoma shule ya awali (maandalizi) Mwera iliyopo Shehia ya Ubago, Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika taarifa kwa waandishi wa habari ya Novemba 21, 2024 ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Daniel Shillah amesema mwili wa mtoto huyo ulikutwa kwenye nyumba ambayo haijakamilika ujenzi.
Kamanda Shillah amesema Novemba 14, 2024 saa moja asubuhi mtoto huyo aliondoka nyumbani kwao kwenda shuleni akisindikizwa na mama yake na baadaye alimkabidhi kijana mmoja ampeleke shule.
“Kijana aliyekabidhiwa naye hakumfikisha shuleni, baada ya kuwaona wanafunzi wengine alimuacha aongozane nao,” amesema.
Kamanda amesema saa saba mchana mtoto huyo hakurudi nyumbani kwao, jambo lililompa wasiwasi mama yake na kwenda shuleni kuuliza.
Amesema shuleni alipewa taarifa kuwa mtoto wake hakufika, ndipo mama huyo alipotoa taarifa Kituo cha Polisi Dunga.
“Ilipofika saa 10:00 jioni huko Mwera vichakani ulionekana mwili wa mtoto huyo kwenye jengo ambalo halijakamilika,” amesema.
Amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi liliendelea na upelelezi uliowezesha kumkamata mtuhumiwa anayedaiwa alimkamata mtoto huyo wakati anakwenda shule, akamziba mdomo na kumuingiza kwenye jengo hilo alikomwigilia kimwili hadi kifo chake.
Kamanda amesema jeshi linaendelea na upelelezi wa shauri hilo na baada ya kukamilika jalada litapelekwa Ofisi ya Wakili wa Serikali kwa hatua nyingine za kisheria.
Mama wa mtoto huyo (jina linahifadhiwa) anayejishughulisha na biashara ya kuuza uji amesema aliamka mapema akamuamsha mtoto wake ili kujiandaa kwa ajili ya kwenda shule.
Amesema alimsindikiza na wakiwa njiani mtoto alimwambia amesahau pesa yake nyumbani ikabidi warudi.
Anaeleza njiani alikutana na mkwewe (mtoto wa kaka wa mumewe), akamwachia mtoto ampe pesa na baadaye amsindikize shuleni.
“Kijana huyo alirudi na kuja kuniambia ameshafika shuleni ila baada ya kufika saa tano mchana hajarudi na si tabia yake, ikabidi nimuulize tena yule kijana, umemuacha wapi hapo ndipo alipodai alimuacha msikiti mdogo,” amesema.
Amesema alioongozana na wapangaji wenzake kwenda kumtafuta mtoto shuleni na baadaye kutoa taarifa polisi.
Baada ya kutoa taarifa Polisi anasema walirudi nyumbani kusubiri majibu, ndipo alipofika mtu na kueleza mtoto ameonekana wakaenda kumuona.
Amesema walipofika walikuta mkusanyiko wa watu na mtoto akiwa tayari ameshafariki dunia.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe Juma ameeleza kusikitishwa na tukio hilo, huku akilipongeza Jeshi la Polisi kwa kutoa ushirikiano na kufanya upelelezi wa haraka uliowezesha mtuhumiwa mmoja wa tukio hilo kukamatwa.