KOCHA msaidizi wa Namungo FC, Shadrack Nsajigwa, amewataja Shomari Kapombe na Yao Kouassi Attohoula kuwa ndio mabeki bora wa kulia hivi sasa ndani ya Ligi Kuu Bara.
Nsajigwa ambaye alishawahi kuwa nahodha wa Yanga na Taifa Stars, ameliambia Mwanaspoti kuwa mabeki hao anawaona wakipita nyayo aliyopita yeye kutokana na aina ya uchezaji wao.
Mbali na hao, pia Nsajigwa amemtaja beki wa kushoto aliyewahi kuitumikia Azam FC, Bruce Kangwa kuwa miongoni mwa nyota wazuri aliowashuhudia katika nafasi hiyo.
“Sio rahisi kufananisha uchezaji wangu wa miaka hiyo na miaka ya sasa, lazima kutakuwa na utofauti, kwa upande wangu naona Kapombe na Yao wana uwezo mkubwa,” alisema na kuongeza:
“Sitaki kulinganishwa nao lakini kwa uwezo walionao nafurahishwa na aina ya uchezaji wao, mfano Kapombe ni mchezaji ambaye amefanya vizuri kwa zaidi ya misimu sita, kitu ambacho sio wachezaji wote wanakiweza, hivyo hivyo kwa Kangwa kafanya vizuri misimu yake yote aliyokuwa Azam FC.”
Kuhusu Yao ambaye huu ni msimu wa pili yupo ndani ya Yanga, Nsajigwa alisema alivyotua tu nyota huyo alifanya vizuri na kuthibitisha kuwa yeye sio mchezaji wa mazoezi pekee bali ana uwezo.
“Kuna wachezaji ambao mazoezi ndio kipimo cha ubora wao na kuna wale uwezo wao unatokana na vipaji vya kuzaliwa navyo, ndio kama Yao, naamini hata akiendelea kubaki ndani ya Yanga kwa zaidi ya misimu minne mbele ataendelea kuonyesha ubora,” alisema Nsajigwa.
Akimzungumzia Kapombe kudumu kwa ubora muda mrefu, Nsajigwa alisema: “Ujue kuna wadau wa mpira wanaweza kumchukia mtu bila hata sababu kisa tu wamemsikia muda mrefu akiwika ndilo linalomkuta Kapombe lakini kwenye suala la uwezo bado anafanya vizuri, kwa upande wangu mimi ni shabiki wake, namfuatilia, naona uwezo wake wa miaka yote ni ule ule.”
Kapombe anayekipiga Simba, amebakiza miezi sita kumaliza mkataba wake sawa na Yao ambaye anacheza Yanga wakati Kangwa alikuwa anaitumikia Azam FC akihudumu kwa zaidi ya misimu mitatu.
Kangwa alijiunga na Azam FC, Agosti 6, 2016 akitokea The Highlanders ya nchini kwao Zimbabwe, amecheza Azam kwa misimu saba kabla ya Julai Mosi 2023 kuondoka.
Kwa upande wa Kapombe, amekuwa ndani ya Simba tangu Julai 2017 alipojiunga na timu hiyo akitokea Azam FC ambapo amefanikiwa kuipa mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu Bara 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021.
Pia amekuwa sehemu ya mafanikio ya timu hiyo kucheza robo fainali tano katika misimu sita ya michuano ya kimataifa ya CAF ngazi ya klabu tangu 2018-2019 hadi 2023-2024.