Rupia atoa tahadhari kwa mastaa Singida Black Stars

WAKATI kikosi cha Singida Black Stars kikijiandaa na mchezo wa Novemba 24 mwaka huu ugenini dhidi ya Tabora United kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mshambuliaji wa timu hiyo, Elvis Rupia amesema wanahitaji kuonyesha bado wako katika mbio zao za ubingwa.

Kauli ya nyota huyo raia wa Kenya imejiri baada ya kikosi hicho kushindwa kupata ushindi katika michezo miwili mfululizo iliyopita kufuatia kupoteza mbele ya Yanga bao 1-0, Oktoba 30, kisha mechi ya mwisho kulazimishwa suluhu na Coastal Union Novemba 2.

“Tumekuwa na muda mzuri wa kupumzika kwa takribani wiki mbili na sasa tunapaswa kuhakikisha tunafanya vizuri ili kurejea kileleni na kupigania ubingwa, haitokuwa rahisi kutokana na ushindani uliopo ingawa hatuna budi kufanya hivyo,” alisema Rupia.

Nyota huyo mwenye mabao matatu katika Ligi Kuu Bara hadi sasa akiwa na timu hiyo, alisema baada ya michezo miwili walikaa kwa pamoja wao kama wachezaji na benchi la ufundi, ili kuweka mikakati mizuri ya kuhakikisha hawadondoshi pointi kizembe.

“Tunahitaji umakini kwa sababu muda ni mchache na ukiangalia ratiba sio rafiki kwetu, tuna michezo migumu ambayo sisi wachezaji wote tunahitaji pia kujipanga ili tusiruhusu kupoteza pointi kama tulivyofanya kwa Yanga na Coastal Union.”

Rupia alijiunga na kikosi hicho msimu wa 2023-2024 akitokea Police FC ya kwao Kenya ambapo alifunga mabao 27 na kuivunja rekodi iliyochukua miaka 47, katika Ligi Kuu ya Kenya ya Moris Aloo Sonyi aliyefunga 26, mwaka 1976 akiwa na Gor Mahia.

Katika msimu wake wa kwanza, Rupia alichezea timu mbili tofauti akianza Singida Fountain Gate kisha dirisha dogo akatua Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na kwa msimu mzima alifunga jumla ya mabao sita akiwa na klabu zote mbili.

Timu hiyo iliyopo nafasi ya tatu na pointi zake 23, baada ya kucheza michezo 10 ikishinda saba, sare miwili na kupoteza mmoja, inakabiliwa na ratiba ngumu kwani itakuwa na wiki moja ya kucheza mechi tatu, kati ya hizo mbili ni za ugenini.

Wikiendi hii Singida itasafiri kwenda Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora kucheza na Tabora United Novemba 24, itaifuata Azam FC Novemba 27, kisha itarudi nyumbani CCM Liti kucheza na Simba Desemba 1.

Related Posts