Dar es Salaam. Shughuli za kibiashara katika maeneo yanayozunguka jengo la ghorofa nne lililoporomoka Kariakoo na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali za mamilioni zimeanza kurejea.
Jengo hilo liliporomoka asubuhi ya Jumamosi Novemba 16, 2024 na mpaka jana Jumatano, vifo vilikuwa vimefikia 20 na majeruhi zaidi ya 86. Tangu siku hiyo, shughuli mbalimbali zilisimama ili kupisha uokoaji.
Barabara na zinazopita na karibu na eneo hilo mathalani za Narung’ombe, Msimbazi, Manyema na Kongo zilifungwa sawia na maduka ya maeneo hayo.
Majeruhi waliokuwa wakiokolewa walikuwa wanapelekwa hospitali mbalimbali zikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Hospitali ya Rufaa ya Amana.
Wafanyabiashara wa maeneo ambayo maduka yao yalifungwa hawakukaa majumbani bali tangu jengo hilo lilipoporomoka walikuwa maeneo hayo. Wapo waliokuwa wakisubiri hatima ya lini wataanza shughuli zao na wengine walisaidiana na vikosi vya dola katika uokozi.
Jana Jumatano, Rais Samia Suluhu Hassan alitembelea eneo hilo, pamoja na kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliofikwa na kadhia hiyo, akitaka biashara ziendelee kwa maeneo ambayo hayako karibu na jengo hilo, huku uondoaji wa mizigo iliyokuwa ndani ya jengo ukiendelea.
Asubuhi ya leo Alhamisi, Novemba 21, 2024, Mwananchi limefika maeneo hayo na kukuta bado maduka yamefungwa hadi mchana ndipo biashara zikarejea na kuanza kwa pilika pilika za kama zamani.
Kwenye jengo lililoporomoka, mizigo ilitolewa na kupelekwa maeneo ambayo yataelezwa na Serikali ambako wahusika watakwenda kuichukua kwa utaratibu maalum.
Awali, kabla ya kufunguliwa kwa eneo hilo ambalo lilikuwa limezungushiwa utepe kuzuia mtu yeyote kwenda ama kupita, wafanyabiashara walikuwa wakiomba kibali kwa askari waliokuwapo kwenda kwenye maduka yao kufungua na kuchukua vitu vilivyokuwamo ndani.
Miongoni ni fedha na mizigo ya wateja wao waliokwisha kuchukua fedha wakisubiri kutumiwa mikoani ama waliokuwa wanafika kuichukua wenyewe.
“Hili jambo limetuumiza watu wote na hususani sisi wafanyabiashara ambao tunatumia haya majengo. Hili tukio limetokea ghafla wakati tulishachukua oda za watu na mteja anasumbua kwa hiyo tunakwenda kuomba kwa askari wakituruhusu tunaingia hapo,” amesema Felix Sanga.
Doris Mshana mwenye meza ya mitandio mtaa wa Muhonda amesema hali hiyo imemuathiri, kwa sababu anatakiwa kupeleka pesa ya mchezo kila siku Sh30,000.
“Muda huu (ilikuwa mchana) nimefungua angalau nipate cha kupeleka nipo hapa tangu asubuhi baada ya jana Rais Samia kutoa kauli ya kuwa tufungue biashara lakini tulipofika tumekuta askari na wakasema haturuhusiwi kuingia ikabidi tutulie,” amesema Doris.
Mmoja wa asakari ambaye hakujitambulisha amesema kwenye kazi kunakuwa na mamlaka, Rais ametoa amri ambayo inakwenda kwa watendaji wake ambao wanatakiwa kufikisha ujumbe kwa watu wa chini.
“Hatuna tatizo endapo tutaambiwa tuwaachie kufanya kazi zao lakini kwa sasa tunasubiri amri kutoka kwa wasimamizi wa eneo hili wakiruhusu sisi hatuna tatizo kwenye hili, na ndiyo maana wale waliokuwa na shida kwenye maduka yao tulikuwa tunawaruhusu,” amesema. Hii ilikuwa saa 5 asubuhi.
Wakati shughuli za kuondoa mizigo na vifusi likiendelea katika eneo hilo Hospitali ya Amana mwili mmoja kati ya miili 20 bado haujachukuliwa na umeendelea kuhifadhiwa katika hospitali hiyo.
Akizungumza na Mwananchi, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, Dk Bryceson Kiwelu amesema hadi kufika leo, miili yote iliyokuwa imehifadhiwa hospitalini hapo imetambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao.
Dk Kiwelu, amesema mwili uliosalia ni kati ya ile tisa iliyorejeshwa baada ya kuagwa Mnazi Mmoja licha ya kuwa ndugu tayari wameshautambua ila wanaendelea na taratibu za mazishi na wakishakamilisha watawakabidhi.
“Tunashukuru ndugu wameshachukua miili yao iliyotokana na ajali ile na hadi kufika leo tumebakiwa na mwili mmoja tu,” amesema Dk Kiwelu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Shirika la Hifadhi ya Taifa (Tanapa), Jenerali Mstaafu, George Waitara akiambatana na Kamishna wa Uhifadhi Tanapa, Musa Kuji amesema inasikitisha kwa jengo kuporomoka kwani limesababisha maafa makubwa ya vifo.
“Maafa makubwa ni vifo vya wenzetu Watanzania na sijui kama wengine sio Watanzania waliopatikana na kwa sababu wokozi bado unaendelea hatujui kama kuna wengine na imesababisha majeruhi,” amesema Waitara.
Amesema wengine inawezekana wameathirika kisaikolojia kwa sababu ya mshtuko wakiwepo ndugu, marafiki na jamaa kwani watu 20 kupotea si jambo dogo.
Kutokana na hilo amesema Tanapa ni sehemu ya wananchi na wameguswa na kutoa Sh20milioni kama msaada kuendelea na shughuli ya ukoaji na kuhudumia waathirika kama wengine walivyotoa msaada.
Hata hivyo, amesema zoezi hili limeratibiwa vizuri tofauti na zamani kila mmoja alikuwa anatoa taarifa yake lakini kwa safari hii inatolewa taarifa kwa utaratibu maalumu na kutokuwepo na taharuki kwa kinachoendelea.
“Taarifa nyingine zinaweza kusababisha taharuki na hasira na ndio maana wananchi nao wametulia kwa kuona Serikali inachokifanya katika kupambana na janga hili kwa mengine sisi hatuwezi kujua kwa sababu Serikali inafanya uchunguzi au itafanya uchunguzi na wananchi watajua nini kimesababisha tatizo hili,” amesema Waitara.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dk Jim Yonazi amesema wamepokea mchango wa kifedha kwani wanahitaji msaada kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Dk Yonazi amewahakikishia Tanapa mchango waliotoa utaenda kutumika kama unavyotakiwa na Serikali ipo makini kuhakikisha inapokea misaada kupitia akaunti maalumu na fedha hizo zinatumika mahususi kwa tukio lenyewe.
“Tunawashukuru kwa namna ambavyo hata bila kubidishwa ninyi mmeona haja ya kuja kuona eneo la tukio, lakini vilevile kushirikiana nasi katika kurejesha hali ya wananchi wetu, msaada huu ni mkubwa hakuna chochote kidogo, kinachopatikana kinafaa,” amesema.