Handeni. Kombo Mbwana, mmoja wa maofisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Tanga, hivi karibuni alikamatwa na kushtakiwa kwa kesi ya jinai inayojumuisha mashitaka matatu chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.
Kombo alifunguliwa mashitaka katika Mahakama ya Wilaya ya Tanga, kwa makosa ya kushindwa kusajili laini ya simu ambayo awali ilikuwa inamilikiwa na mtu mwingine na kushindwa kuripoti kuhusu mabadiliko ya laini hiyo.
Lakini kabla ya kesi hiyo, itakumbukwa Kombo alitoweka nyumbani kwake tangu Juni 15, 2024, baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana kwa madai kuwa alikuwa akijenga nyumba kwenye kiwanja kinachodaiwa kilishauzwa kwa mtu mwingine.
Watu hao walipofika nyumbani kwake walimtaka aende kwenye gari walilokuja nalo ili akawaonyesha nyaraka za umiliki wa kiwanja hicho, lakini badala yake walimchukua na kuondoka naye kuelekea kusikojulikana.
Familia yake na watu wengine walipaza sauti kumtafuta kwani baada ya hapo hakujulikana yupo wapi.
Hata hivyo, Julai 14, 2024, Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, kupitia Kaimu Kamanda Zakaria Bernard, lilitangaza kuwa linamshikilia kwa tuhuma za makosa ya kimtandao. Siku mbili baadaye, Julai 16, 2024, alifikishwa mahakamani.
Novemba 20, 2024, Mahakama ya Wilaya ya Tanga ilimhukumu kifungo cha siku 15 gerezani au kulipa faini ya Sh85,000 ambazo alizilipa na kuachiwa huru, ikiwa ni zaidi ya siku 150 za misukosuko tangu alipotoweka.
Asimulia masahibu aliyokumbana nayo
“Niliamka saa mbili asubuhi, nilikuwa na safari ya kwenda Tanga tulikuwa na uzinduzi wa tukio la kusajili wanachama wa Chadema kidijitali. Kabla sijatoka mke wangu akaniambia nje kuna mtu anazungukazunguka, nilichungulia dirishani kuangalia kama ninamjua lakini sikumfahamu, hivyo nilitoka nje,” anasimulia Kombo alipozungumza na Mwananchi leo Alhamisi Novemba 21, 2024 akiwa nyumbani kwake Handeni mkoani Tanga.
Anasema alipotoka nje akiwa amevaa pensi na sweta, alikutana na mtu aliyekuwa anazunguka kwenye uwanja wa nyumba yake.
Ndipo mtu huyo akamwambia eneo alilojenga ni lake na aliuziwa na mzee mmoja hapo Sindeni ambaye ana watoto pacha.
“Kwa kuwa nilikuwa nataka kumjua huyo mzee kwa undani, nikajikuta naingia mtegoni, nikawa nimempa nafasi yule mtu ya kunihoji maswali zaidi,” anasimulia Kombo.
Anasema akamwambia waongozane naye kwenye gari lililokuwa limeegeshwa jirani na nyumbani kwake akamuonyeshe nyaraka.
“Tulipofika kwenye gari nikakamatwa na kuingizwa ndani ya gari hilo, nikafungwa kitambaa usoni na mikononi nikafungwa pingu safari ikaanza, sikujua tunaelekea wapi,” anasema Kombo.
Anasema walitembea kama dakika 10 hivi gari likasimama akasikia mlango unafunguliwa kisha ukafungwa na gari likaondoka kwa kasi.
“Kuna mahali tulifika gari likasimama nikafunguliwa kitambaa nilichofungwa usoni, lakini sikutambua ni eneo gani nikashushwa na kuingizwa kwenye nyumba moja ambayo sikuitambua pia,” anasema.
Anasema kitu cha kwanza alichoambiwa na watesi wake ni namba za siri za simu zake alizokuwa nazo lakini aliwagomea akitaka mpaka awepo mwanasheria wake, kauli iliyoamsha hasira na kuanza kupigwa na alipoona mateso yamezidi akatoa namba za siri za simu zake zote.
Anasema ndani ya siku zote 29 alizokuwa akihama hama nyumba huku amefungwa kitambaa usoni na pingu mkononi, hakufahamu wapi alipo.
Anasema licha ya mateso yote, lakini watu hao walikuwa wakimpatia chakula na kuna wakati aliugua, walimtibu pia kumpatia dawa na ilifikia wakati akatundikiwa maji (drip) kutokana na homa kali iliyompata.
“Nilikuwa naishiwa nguvu, nikatundikiwa drip nadhani ilikuwa ya maji japo sikuiona na wakanichoma sindano kwa kuwa waliniambia naumwa malaria,” anasema Kombo.
Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na Daktari wa macho kutoka Hospitali ya Mnazi Mmoja, Neema Moshi aliyesema kuwa mtu mzima akifungwa macho kwa muda wa siku 15, hawezi kupata athari yoyote.
Huku Daktari bingwa wa macho kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili – Mloganzila, Anna Sanyiwa akisema, “Kama ni mtu mzima na macho hayakukandamizwa, hawezi kupata tatizo lolote.”
Kombo anasema baada ya kuhukumiwa na kulipa faini iliyomrejesha uraini anamshukuru Mungu ameikuta familia yake ikiwa salama.
Hata hivyo Kombo anasema mambo yake mengi yameharibika hivyo kuathirika kiuchumi.
“Familia yangu imeathirika kisaikolojia, lakini kitu kikubwa nimeanguka kiuchumi kwa sababu kuna vitu niliviacha nimerudi sijavikuta kwa sababu familia ilikuwa inapambana kuhakikisha watoto wanakula, hivyo walikuwa wakiuza pia baadhi ya mali ili wapate fedha ya kujikimu,”amesema
Anasema mifugo yake yote zikiwamo mbuzi zaidi ya 20 alizokuwa anafuga zimepotea zingine kwa kuibiwa.
“Nyumbani kwangu kwa nyuma nilikuwa na mabanda ya kuku zaidi ya 200, lakini sijakuta hata mmoja, nimeathirika zaidi kiuchumi,”anasema Kombo.
Alalama namna alivyokamatwa
Kombo anasema licha ya kukiri kosa aliloshtakiwa nalo, lakini amelalamikia utaratibu uliotumika kumkamata kuwa haukufuatwa na haukuzingatia sheria, huku akisema jambo hilo amewaachia wanasheria wake walishughulikie.
“Nimeacha kazi kwa wanasheria, mimi sikirii kufanya kitu, ila namuachia Mungu kwa sababu niliamini kesi hii alinipa Mungu na ndiye aliniondolea,” anasema Kombo.
Anasema anaamini kila jambo linapokuja kwa binadamu lina mwanzo na mwisho wake huku akisema kama ilifikia hatua haikujulikani alipo na ikafahamika na kupelekwa mahakamani, huenda ni miujiza ya Mungu.
“Baada ya kuja mahakamani nikapewa dhamana na sasa niko huru na jana (juzi) nimefungwa kifungo cha siku 15, au kulipa faini ya Sh85,000 nikalipa, naamini ilikuwa mwanzo na limefika mwisho,”anasema Kombo.
Anasema anamshukuru Mungu kwa uzima na mali na mambo mengine yote yanatafutwa huku akieleza misuguano hiyo inahusiana na masuala ya kisiasa.
Anadai nia aliyoonyesha ya kutaka kugombea Jimbo la Handeni Vijijini mwaka ujao ni turufu ya watesi wake kumuingiza katika mapito hayo.
“Asilimia 100 kwa upande wangu naona siasa kwa sababu siku zote huko ni kama timu za mpira za Simba na Yanga, hazitamani timu ndogo zipande daraja, hata kwenye siasa iko hivyo, wakubwa hawatamani wadogo wapande,” anasema Kombo.
Anasema baada ya kuonyesha nia ya kugombea jimbo hilo alishaanza kufanya maandalizi ndani ya chama hicho kabla ya kutiwa mbaroni na Jeshi la Polisi kutokana na tuhuma hizo.
“Inahusiana kabisa na siasa kwa sababu mimi ni mwanasiasa na ni mkosoaji na hata mazingira niliyochukuliwa kama ningekuwa na uhalifu huo ningeweza kuzuiliwa.
“Kuna wahalifu wengi wanakamatwa kawaida tu, lakini nikitazama makosa yangu na aina ya ukamataji ni tofauti, ndiyo maana nasisitiza sababu kubwa ni za kisiasa, mwaka 2025 kama chama changu kitaridhia ninataka kugombea ubunge kwa hiyo kuna watu, hawataki na wananihofia,” anasema Kombo.
Anadai watesi wake hawawezi kutoka ndani ya chama chake kwani kinaamini katika viongozi vijana.
Akizungumza na Mwananchi, Mariam Rajabu mkewe na Kombo anasema baada ya miezi mitatu kupita bila kuwepo dalili ya mume wake kuachiwa, ilibidi arudi nyumbani kwa wazazi wake.
Anasema alichukua uamuzi huo baada ya kuona mazingira ya nyumbani kwake ni magumu kwa kuwa kuna muda alikosa hata fedha ya chakula.
“Baada ya kuona mazingira ya hapa kwangu ni magumu ilibidi nirudi kwetu, maana kuna wakati mtoto alikuwa anaumwa na pesa sina. Leo nimerudi kwangu mume wangu amerudi,” anasema Mariam.
Naye Hellena Joseph mama mzazi wa Kombo anasema mpaka sasa wametumia zaidi ya Sh3 milioni katika kufuatilia kesi ya Kombo.
“Tumeuza mashamba, baiskeli, kuku na pesa nyingine tumekopa kwa watu na sasa tuna madeni kutokana na hili, hivyo kumalizika kwa kesi hii ni nafuu kubwa kwetu kama familia,” anasema Hellen.