Taasisi za umma, sekta binasi Musoma zapewa siku 40

Musoma. Mkuu wa Wilaya ya Musoma, mkoani Mara, Juma Chikoka amezitaka taasisi za umma na binfasi zinazotoa huduma ya chakula kwa watu kunzia 100 kuendelea kuhakikisha wanaanza kutumia nishati safi ya kupikia kabla ya Desemba 31, 2024.

Chikoka ametoa wito huo baada ya kubaini taasisi nyingi wilayani humo bado hazijaanza mchakato wa kuhama kutoka katika matumizi ya nishati ya mkaa na kuni kuelekea katika matumizi hayo ya nishati safi na salama ya kupikia licha ya kutakiwa kufanya hivyo.

Akizungumza leo Alhamisi Novemba 21, 2024 mjini Musoma wakati wa ziara ya kutembelea taasisi za umma na binafsi kuhimiza juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, Chikoka amesema jamii inapaswa kuondokana na dhana kuwa matumizi ya nishati safi ni gharama kubwa kulinganisha na gharama za matumizi ya nishata zinazotumika hivi sasa.

Ametolea mfano wa Shule ya Sekondari ya Mara ambayo tayari imeachana na matumizi ya kuni kwa ajili ya kupikia ambapo amefafanua baada ya kuweka mfumo wa gesi shule hiyo hivi sasa inatumia Sh3.2 milioni kwa mwezi kutoka Sh4.6 milioni zilizokuwa zikitumika kwa ajili ya manunuzi ya kuni.

“Huu ni mfano hai kabisa nishati safi ni nafuu kuliko tunavyodhani lakini pia ina faida nyingi sana kiafya na kimazingira tofauti na haya matumizi ya kuni na mkaa kwani mbali na kuharibu mazingira lakini pia maisha hasa ya wapishi yako hatarini kwani kwao ni rahisi kupata magonjwa ya kifua na mengine mengi,” amesema Chikota.

Kunzia leo Alhamisi hadi Desemba 31, 2024 ni sawa na siku 40 kwa taasisi ambazo zimeelekezwa na DC Chikota. Agizo kama hilo lilitolewa na mkuu wa nchi, Rais Samia Suluhu Hassan, Mei 8, 2024, alipozindua mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia wa mwaka 2024/2034 alitoa marufuku ya matumizi ya kuni na mkaa kupikia kwa taasisi za umma na binafsi zinazohudumia watu zaidi ya 100.

Hatua hiyo ililenga kuweka msisitizo wa utekelezaji wa mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, unaotaka kufikia mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi.

Mkakati huo unakuja katika kipindi ambacho, takwimu zinaonyesha asilimia 90 za kaya zote nchini zinatumia nishati ya kuni na mkaa. Hiyo ni sawa na kusema kati ya kaya 10, tisa zinatumia nishati isiyo safi kupikia.

Hali hiyo inatajwa kusababisha athari zikiwemo za magonjwa ya upumuaji yanayotokana na uvutaji moshi na kupoteza uhai wa takriban watu 33,000 kwa mwaka.

Katika ziara ya DC Chikota, wapishi shule za Msingi Mwisenge na Nyarigamba A katika Manispaa ya Musoma wameomba kuwekewewa mifumo ya gesi ya kupikia ili waweze kuondokana na changamoto wanazokutana nazo kutokana na matumizi ya kuni wakati wa kupika.

Mpishi wa shule ya Msingi Mwisenge, Deborah Mkama, amesema hivi sasa ana tatizo la kifua ambalo anaamini limetokanana moshi wa kuni hivyo kuomba kuboreshewa mazingira ya kazi kwa kuwekewa mfumo wa gesi ili kuondokana na changamoto hiyo.

“Nina ukungu kifuani na umetokana na moshi kwani nimepikia kuni kwa muda mrefu sana kama mnvyoona huu moshi lakini pia gesi itarahisisha upishi kwa ujumla,” amesema Mkama.

Mpishi wa Shule ya Msingi Nyarigamba A, Jenifa Mseti amesema kutokana matumizi ya kuni hivi sasa ameanza kupoteza uwezo wa kuona na kwamba anaamini ili aweze kuendelea na kazi hiyo ni lazima kuwepo kwa nishati salama ya kupikia shuleni hapo.

“Sina uhakika kama nitaendelea na hii kazi kwa miezi mitano ijayo ingawa naipenda na ndiyo kazi ninayoitegema lakini sasa kama unavoona mazingira haya naumia sana na moshi imefika hatua siwezi kuona mbali, naomba kama inawezekana walete gesi hapa,” amesema Mseti.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwisenge, Sigawa Mwita amesema shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 600 inatumia Sh1 milioni kwaajili ya ununuzi wa kuni kila mwezi gharama ambayo ni kubwa zaidi.

Amesema tayari wametenga bajeti kwaajili ya kuweka mfumo ya gesi na kwamba mfumo huo ambao bao unatarajiwa kupunguza gharama za matumizi ya nishati ya kupikia shuleni hapo unatarajiwa kuanza kutumika mwakani.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Musoma, Gabriel Stewart amesema chuo hicho kimepunguza matumizi kutoka Sh5.5 milioni kwa miezi mitatu kwaajili ya ununuzi wa kuni hadi Sh3 milioni kwa miezi minne baada ya kueweka mfumo wa gesi kwaajili ya kupikia chuoni hapo.

Related Posts