Mwanza. Ikiwa imepita siku moja tangu kipyenga cha kampeni za Serikali za Mitaa kipulizwe, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mwanza imewataka wapigakura kutokuwa chanzo cha wagombea kutoa rushwa.
Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 21, 2024, Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Idrisa Kisaka alipozungumza na waandishi wa habari mkoani humo kuelekea uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika nchini Novemba 27, mwaka huu.
Kisaka amesema kutumia kauli ya ‘Unatuachaje sasa’ kuwa miongoni mwa kauli zinazotumiwa na wapigakura kuwaomba rushwa wagombea wakati wa kampeni huku akisema sheria haitomfumbia macho mpokeaji na mtoaji wa rushwa mkoani humo.
“Vipindi vyote vya uchaguzi kwa uzoefu na utafiti (bila kuutaja) wagombea hutumia rushwa kuwashawishi wapiga kura ili wachaguliwe. Pia kuna baadhi ya wananchi wanawashawishi wagombea kwamba unapitaje ama unatuachaje, hayo yote tuko macho kuyafuatilia,” amesema Kisaka.
Kauli hiyo ya Kisaka inaungwa mkono na mkazi wa Igoma jijini Mwanza, Sylvia Sylvester ambaye ameishauri mamlaka hiyo kuweka maofisa wake kwenye mikutano ya wagombea katika uchaguzi huo kwa kile alichodai vitendo vya rushwa vinaendelea maeneo mbalimbali kwenye uchaguzi huu bila wahusika kuchukuliwa hatua.
“Kuzungumza ni suala moja na kuchukua hatua ni jambo jingine. Takukuru wanafanya kazi nzuri tunaamini uchaguzi wa serikali za mitaa na kampeni zake unaweza kuwa mwanzo wa kuonyesha ufanisi wao kwa kutuonyesha watu ambao wamewakamata na kuwachukulia hatua kwa tuhuma za rushwa kwenye uchaguzi,” amesema Sylvia.
Akizungumzia rushwa kwenye uchaguzi huo, Songareli Maduhu ameitaka jamii kujiepusha na vishawishi vya kupokea hongo kutoka kwa wagombea ili kuwapatia kura badala yake wajikite kuangalia ubora wa mgombea husika.
“Maamuzi ya kumchagua kiongozi wa serikali ya mtaa yanaathari za moja kwa moja kwenye uchaguzi mkuu, tujitahidi kuchagua viongozi sahihi bila kusukumwa na rushwa ama vishawishi vya mali,” amesema Maduhu.
Vyama vya siasa vimeendelea na kampeni zake ambapo leo Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) bara, Tundu Lissu akiendeleza kampeni zake mkoani Mara katika Kanda ya Victoria, Chama cha Mapinduzi nacho kikiendelea na kampeni hizo kwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, John Mongela akiwa mkoani Songwe.
Vyama vingine hususan ACT-Wazalendo nacho kinaendelea na kampeni zake ambapo aliyekuwa kiongozi mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe alizindua kampeni za wagombea wake mkoani Tabora.
Katika hatua nyingine, Kisaka amesema katika kipindi cha Julai hadi Septemba 30 mwaka huu Takukuru imefuatilia utekelezaji wa miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh25.8 bilioni na kubaini miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh6 bilioni ina mapungufu madogo madogo.
“Miradi hiyo inatekelezwa katika sekta ya elimu, afya, nishati, barabara, maji na ardhi. Tutaendelea kufanya uchambuzi wa mifumo ya umma ili kudhibiti uvujaji wa mapato ya Serikali na matumizi mabovu ya rasilimali za Umma,” amesema Kisaka.