Katika taarifa, Turk amesema alishtushwa na kutekwa nyara kwa Besigye mnamo Novemba 16, 2024 nchini Kenya na kurejeshwa kwake kwa nguvu nchini Uganda .
Turk ameihimiza serikali hiyo ya Uganda kumwachilia huru Besigye na kuhakikisha kwamba hatua zozote zaidi zinazochukuliwa kukabiliana na tuhuma zinafanyika kwa kuzingatia kikamilifu sheria za kimataifa za haki za binadamu.
Mazingira ya kutekwa nyara kwa Besigye yanapaswa kuchungzwa
Mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, pia amesema lazima kuwe na uchunguzi kamili kuhusu mazingira ya kutekwa nyara kwa Besigye.
Mashtaka dhidi ya Besigye yanaweza kusababisha adhabu ya kifo
Turk ameongeza kuwa Besigye, alizuiliwa kwa mara ya kwanza bila mawasiliano na mtu yeyote kabla ya kufikishwa katika mahakama ya kijeshi mjini Kampalahapo jana na akaonya kuwa mashtaka dhidi ya Besiegye ya kumiliki silaha kinyume cha sheria, pamoja na makosa ya kiusalama yanaweza kusababisha kutolewa kwa adhabu ya kifo.
Turk pia amesema hatua ya kurejeshwa kwa Besigye nchini Uganda , inafuatia kutekwa nyara kutoka Kenya mwezi Julai kwa wafuasi wake wengine 36 ambao baadaye walirejeshwa Uganda na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi.
Mwanasiasa Kizza Besigye wa Uganda apandishwa kizimbani mahakama ya kijeshi
Mkuu huyo wa haki za binadamu amesema utekaji nyara kama huo wa viongozi wa upinzani wa Uganda pamoja na wafuasi wao lazima ukomeshwe, pamoja na kushtakiwa kwa raia katika mahakama za kijeshi.
Kauli zinazotokana na kukamatwa kwa Besigye
Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya Besigye.
Shirika la kimataifa la kutetea haki Amnesty International, nalo limesema hii sio mara ya kwanza kwa mpinzani wa kigeni kutekwa nyara katika ardhi ya Kenya na kuongeza kuwa ni sehemu ya mtindo unaokua na unaotia wasiwasi wa ukandamizaji wa kimataifa.
Mke wa mwanasiasa Besigye asema mumewe ametekwa nyara
Kwa upande wake, serikali ya Kenya imesema kuwa inachunguza ni jinsi gani ambapo mwanasiasa wa upinzani mashuhuri wa Uganda alivyoondolewa kwa nguvu kutoka Nairobi wiki hii, huku kukiwa na ukosoaji mkubwa kwamba imeshindwa kuwalinda wapinzani wa kigeni katika ardhi yake.
Uganda: Wanachama wa chama cha upinzani FDC washtakiwa kwa ugaidi
Huku hayo yakiri, msemaji wa serikali ya Uganda, amesema serikali hiyo haikuhusika katika utekaji nyara wa Besiegye na kwamba kukamatwa kwake nje ya nchi kulifanyika kwa ushirikiano na nchi mwenyeji.