Urusi imefyetuwa kombora la kuvuka mabara leo (Alhamisi) asubuhi kutokea mkoa wake wa kusini wa Astrakhan kuishambulia Ukraine, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kutumia silaha zenye nguvu kubwa namna hiyo tangu ilipoanzisha vita hivyo.
Jeshi la anga la Ukraine ambalo limetowa ripoti hiyo limesema kwamba shambulio hilo la Urusi limeilenga miundo mbinu kadhaa muhimu katika mji wa Dnipro.
Shambulio hilo la Urusi linashuhudiwa ikiwa ni baada ya Ukraine nayo siku ya Jumanne kwa mara ya kwanza kutumia makombora yaliyotoka Marekani na Uingereza kuishambulia Urusi, hatua ambayo Urusi ilishatowa tahadhari miezi kadhaa nyuma, kuionya Ukraine kwamba itazidisha makali kwenye vita hivyo.
Haijakuwa wazi kutoka Ukraine juu ya uharibifu uliofanywa na shambulio hilo la leo la Urusi la kombora la masafa marefu.Soma pia: Korea Kaskazini yarusha kombora la ICBM wakati Marekani, Seoul zikiisokoa kutuma jeshi Urusi
Lakini pia Urusi kupitia msemaji wake wa wizara ya mambo ya nje Maria Zakharova, imesema iko tayari kutafakari juhudi zozote za kweli za kuleta amani katika mgogoro huo na ambazo zitazingatia maslahi yake na hali halisi ya vita hivyo, lakini sio juhudi zenye mirengo ya kisiasa.
Marekani Jumatano ilitangaza inataka kuipelekea Ukraine mabomu ya kutega ardhini ili kuisaidia nchi hiyo kuvirudisha nyuma vikosi vya Urusi.
Hatua hiyo imekosolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human rights Watch kutokana na athari zinazoweza kusababishwa na mabomu hayo kwa raia .
Rais Volodymyr Zelensky amefurahishwa na uamuzi huo wa Marekani akisema mabomu hayo ni muhimu sana katika kuyazuia mashambulizi ya Urusi.
Kufuatia hali inayoendelea hivi sasa kwenye vita hivyo, Hungary imesema itaweka mfumo wa ulinzi wa anga katika eneo lake la Kaskazini Mashariki kutokana na kitisho cha kutanuka kwa vita hivyo kuongezeka kwa namna ambayo haijawahi kutokea.
Jana Jumatano waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Kristof Szalay- Bobrovniczky alisema bado wanaamini amani inaweza kupatikana hivi karibuni kupitia mchakato wa kidiplomasia na sio wa kijeshi lakini pia akasisitiza ni bora zaidi kujiandaa kwa lolote linaloweza kutokea.Soma pia: Vikosi vya Urusi vyadai kusonga mbele upande wa mashariki mwa Ukraine
Wasiwasi wa Hungary waongezeka
Uamuzi huo wa Hungary umefanyika baada ya mkutano wa baraza la ulinzi la nchi hiyo uliotishwa na waziri mkuu Viktor Orban kujadili kinachoendelea sasa katika vita vya Ukraine.
Itakumbukwa kwamba Hungary ni mshirika wa jumuiya ya kujihami ya NATO na pia mwanachama wa Umoja wa Ulaya lakini inagawana mpaka na Ukraine.
Jeshi la nchi hiyo hivi sasa liko kwenye mpango wa kuimarisha uwezo wake huku ikielezwa kwamba baadhi ya vikosi vyake vimeshawekwa katika hali ya tahadhari.
Kwa upande mwingine huko Laos mawaziri wa ulinzi wa mataifa ya Jumuiya ya kanda ya Kusini Mashariki mwa Asia-ASEAN wamekutana leo na naibu waziri wa ulinzi wa Korea Kusini Kim Seon ho amewaambia waandishi habari kwamba kupelekwa kwa vikosi vya Korea Kaskazini nchini Urusi ni kitendo cha uhalifu dhidi ya ubinadamu.