Viongozi SADC warefusha muda wa vikosi vyake Kongo – DW – 21.11.2024

Uamuzi huo wa kuongeza muda wa vikosi vya mataifa ya kusini mwa Afrika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo umefikiwa katika Mji Mkuu wa Zimbabwe, Harare, wakati wa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC uliofanyika hapo jana Jumatano. Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ni miomngoni mwa nchi wanachama 16 wa SADC.

Ujumbe uliotolewa baada ya mkutano huo wa kilele ulielezea hofu ya hali ya kiusalama na kiutu nchini Kongo na kusisitiza dhamira ya jumuiya hiyo kuiunga mkono serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Nchi yenye nguvu katika kanda ya Kusini mwa Afrika, Afrika Kusini, ilituma kikosi cha karibu wanajeshi 3,000 kwa ajili ya huo mpango wa SADC nchini Kongo huku Tanzania na Malawi zilituma zaidi ya wanajeshi 2,000 Disemba iliyopita.

Kikosi cha ulinzi wa taifa cha Afrika Kusini (SANDF) huko mjini Pemba Msumbiji
Kikosi cha ulinzi wa taifa cha Afrika Kusini (SANDF)Picha: ALFREDO ZUNIGA/AFP

Soma: SADC yarefusha muda wa jeshi lake Kongo

Vikosi vya SADC ni sehemu ya vikosi kadhaa vinavyolinda usalama huko mashariki mwa Kongo kuliko na utajiri wa madini. Majeshi ya Kongo, mamluki wa kigeni, kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa na zaidi ya makundi 100 yaliyojihami yanayopigania madaraka, ardhi na madini yamekita kambi katika eneo hilo. Baadhi ya makundi kwenye eneo hilo yanajaribu kuzilinda jamii zao.

Kuongezeka kwa machafuko huko Mashariki mwa Kongo kumepelekea vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa vilivyokuwa vinastahili kuondoka mwezi ujao, kuendelea kusalia. Waziri wa mawasiliano wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Patrick Muyaya amesema kutatolewa tarehe mpya ya vikosi hivyo kuondoka, ingawa hakutoa taarifa zaidi.

Nchi jirani ya Rwanda imekanusha madai yaliyotolewa na serikali ya Kongo na wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwamba inaliunga mkono kundi la waasi wa M23 huko mashariki mwa Kongo. Kongo na SADC kuanzisha operesheni ya pamoja

Ama kuhusiana na matokeo ya uchaguzi yaliyosababisha machafuko Msumbiji na vifo vya watu 30, viongozi hao wa SADC wameelezea dhamira yao ya kushinikiza suluhisho la amani. Viongozi hao lakini hawakutoa taarifa zaidi kuhusiana na jinsi watakavyosaidia kuleta amani nchini humo.

Kikosi cha ulinzi wa taifa cha Afrika Kusini (SANDF) mashariki mwa Kongo
Kikosi cha ulinzi wa taifa cha Afrika Kusini (SANDF) mashariki mwa KongoPicha: AUBIN MUKONI/AFP

Tume ya uchaguzi nchini Msumbiji ilitangaza ushindi kwa chama tawala Frelimo na mgombea wake wa urais Daniel Chapo katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 9. Chama cha Frelimo kimeiongoza Msumbiji tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Ureno mwaka 1975.

Venancio Mondlane, mgombea huru ambaye alikuwa wa pili kwa kupata asilimia 20 ya kura za kitaifa, amepinga matokeo hayo mahakamani na kuitisha maandamano kote nchini humo.Marais wa jumuiya ya SADC waidhinisha kupelekwa jeshi Kongo

Mahakama ya Juu ya Msumbiji bado haijatoa uamuzi kuhusiana na kesi ya kupinga matokeo iliyowasilishwa na upinzani. Rais anayeondoka mamlakani Filipe Nyusi amesema kwamba yuko tayari kukutana na wagombea urais katika uchaguzi uliopita ili kusuluhisha mivutano ya kisiasa inayoshuhudiwa.

Vyanzo: Reuters/AP

 

Related Posts