Na Said Mwishehe,Michuzi TV
KATIBU wa Halmashauri Kuu(NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi,Uenezi,Siasa na Mafunzo CPA Amoss Makala amesema nafasi za uenyekiti wa mitaa,vijiji na vitongoji ni kazi ya utumishi wa umma, hivyo watakaochaguliwa na kushinda uchaguzi huo wanapaswa kuwa karibu na wananchi wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Hivyo amesema wagombea wa Chama hicho watakaoshinda baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa,vijiji na Vitongoji utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu watatoa ushirikiano kwa wananchi kwa lengo la kuhakikisha wanatatua changamoto katika mitaa wanayotoka.
CPA Makala ameyasema hayo leo Novemba 21,2024 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kampeni ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa baada ya chama hicho kuzindua kampeni zake jana nchini kote.
“Uchaguzi wa Serikali za mitaa unaokwenda kufanyika Novemba 27 mwaka huu ni uchaguzi muhimu maana viongozi wanaotokana na uchaguzi huo wanakwenda kushughulika na changamoto za wananchi.
“Hivyo CCM tumeweka wagombea wenye sifa na waliotayari kuwatumikia.Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wanakwenda kufanya kazi ya utumishi wa umma, hivyo kuwa na viongozi wenye sifa ni jambo la msingi na Chama chetu kimezingatia hilo,” amesema CPA Makala.
Aidha amesema CCM itashinda kwa kishindo katika uchaguzi huo wakati baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani, akiwataka Watanzania kutopata shida katika kufanya uamuzi sahihi wa kukipa kura chama hicho tawala.
Pia CPA Makala amewakumbusha viongozi wa
CCM kuwa ifikapo Novemba 24 wakumbusheni Mwananchi wote waliojiandikisha kupiga kura kwani kupiga kura ndio kunawezesha wagombea wao kushinda.