Watoto wanne kati ya 15 wa Neema wapata ufadhili wa masomo

Morogoro. Hatimaye watoto wanne kati ya 15 wa marehemu Neema Kenge (39) wamepata ufadhili wa kusomeshwa shule ya bweni na Kituo cha Buloma Foundation iliyopo Kibaha mkoani Pwani, baada baba wa watoto hao kuomba msaada kutokana na kuzidiwa majukumu.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Novemba 21, 2024 Ofisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Mbuyuni, Alicia Mbaga amesema uongozi wa kituo hicho umejitokeza juzi ambapo tayari wameshafanya mazungumzo na baba wa watoto hao ambaye ameridhia watoto wake hao kwenda kusomeshwa.

Watoto waliopata ufadhili wa kwenda kusoma Buloma Foundation ni pamoja na Elia, Prisca, Maryy na Sarah.

“Jana niliitembelea familia na tayari tumeshakubaliana watoto wanne watakwenda kusomeshwa Kibaha, Serikali tumekishukuru hiki kituo kwa kuwa kitawafanya watoto hawa wawe kwenye mazingira salama, kuliko ilivyo sasa kwani muda mwingi hasa usiku baba yao anakuwa kwenye shughuli zake za ulinzi,” amesema Mbaga.

Ameongeza, “Kwa sasa bado wapo kwenye hali si mbaya, sababu bado watu wanakwenda kuwaona na kutoa pole na rambirambi lakini naamini itafika mahala hizi pole na rambirambi zitakata na ndio kutakuwa na hali ngumu sana ya maisha maana kwa kweli yule mama yao (marehemu) alikuwa anahangaika na kila aina ya vibarua ili apate chakula cha watoto wake sasa hayupo.”

Mbaga amesema pamoja na ufadhili huo, bado ofisi inaendelea kutafuta wadau wengine waweze kusaidia mahitaji ya msingi kama chakula, mavazi kwa watoto wadogo ambao umri wao bado haujafikia kwenda shule.

Awali, baba wa watoto hao, Thomas amesema kuwa pamoja na ufadhili huo lakini bado anahitaji msaada wa maziwa pamoja na unga wa lishe kwa ajili ya mtoto wake mdogo wa miezi tisa ambaye alisitishwa kunyonya baada ya mama yake kufariki dunia.

“Kwa kweli hali yangu ya maisha sio nzuri lakini sasa nitafanyaje na mimi ndio baba, nimeshaachiwa watoto itabidi nipambane tu kwa namna yoyote wapate chakula. Huyu mdogo ndiye anayeniumiza kichwa maana gharama ya maziwa kila siku sitaweza kumudu, kwa sasa anakula chakula chochote kinachopatikana iwe ugali, uji tunampa.”

Ametaja msaada mwingine anaohitaji kuwa ni (pampasi) kwa ajili ya kuzuia mkojo kwa kuwa mtoto huyo mdogo bado hajaweza kujitambua na kuzungumza hivyo muda mwingi amekuwa akijisaidia.

“Analelewa na dada zake hawa watatu, nao wana watoto wadogo sasa kuna wakati dada zake wanaelemewa na malezi, lakini nikipata pampasi zitasaidia kupunguza kazi ya kufua nguo za haja ndogo.

“Naomba ndugu zangu Watanzania wanisaidie napita kwenye wakati mgumu, yaani nikipata hata kiroba cha unga maharage, dagaa nitashukuru,” amesema Thomas.

Mtoto wa pili katika familia ya watoto hao 15, Thomas Simon (19) amesema kituo kilichojitokeza kusaidia wadogo zake hao wanne ni kile kile alichokuwa akilelewa yeye, tangu akiwa mdogo mpaka sasa amemaliza kidato cha nne.

“Mwanzo kituo hiki kilinichukua mimi na kaka na dada zangu wawili lakini wenzangu walishindwa kuendelea na masomo wakarudi Morogoro, nilikomaa mpaka kumaliza kidato cha nne, huyu kaka angu yeye aliacha shule akisema haelewi lakini dada zangu walishindwa kuendelea kusoma na waliporudi walipewa ujauzito na wanaume ambao hawafahamiki,” amesema Simon.

Amesema kitendo cha kituo hicho kutaka kuwachukua wadogo zake na kuwasomesha yeye ameridhia na ameshukuru kwa sababu anajua watapata malezi mema na elimu bora ambayo itakuja kuwasaidia.

Thomas amesema kwa sasa ameshamaliza kidato cha nne na amerudi nyumbani kwao, hivyo amewaomba wasamalia wema wamsaidie kupata kazi ili aweze kujihudumia na wadogo zake.

“Nimemaliza kidato cha nne mwaka jana, niliendelea kubaki kwenye kituo lakini kutokana na utaratibu wa kituo hiki kwa sasa natakiwa kuondoka pale kituoni ili niweze kujiendesha mwenyewe ijapokuwa mpaka sasa sijapata kazi, nimerudi hapa nyumbani siku chache kabla ya mama kufariki dunia yaani hapa nilipo sielewi kabisa maana maisha ya hapa nyumbani ni changamoto,” amesema Simon.

Simon amesema ndoto zake ni kuwa askari polisi au wa JWTZ na kwamba alishajaribu kuomba nafasi za majeshi zilipotoka lakini hakubahatika kuchaguliwa kujiunga.

Anasema pia ana kipaji cha kucheza mpira na ana kipaji lakini bado hajapata wadau wa kumshika mkono apate timu za maana, kwa sasa anachezea timu za mtaani tu ambazo hazina maslahi yoyote.

Simon mesema kutokana na hali ngumu ya maisha iliyopo nyumbani kwao, anaomba wadau wamsaidie kupata kazi yoyote itakayomsaidia kujikwamua na hali ngumu aliyonayo.

Msaada mwingine anaoomba mtoto huyo kwa wadau na wasamaria wema ni kuboreshewa makazi kwa kuwa nyumba wanayoishi imechakaa na pia ni nyumba ya urithi ambayo wanaishi familia nzima.

“Yaani hii nyumba unayoiona mwandishi licha ya kuchakaa kiasi hiki tunaishi familia kina shangazi pia. Hapa tuna vyumba viwili tumekuwa tukilala chumba kimoja watoto sita hadi saba wa rika tofauti na hata watoto wa kike nao kwenye chumba chao wanalala hivyo hivyo tena kila chumba kina kitanda kimoja tu, baba yeye muda wa usiku anakuwa kwenye kazi zake za ulinzi,” ameongeza.

Wakati wa uhai wake, mama yao Neema alifanikiwa kuzaa watoto hao 15 kwa baba mmoja ambaye ni Simon Thomas na moja ya vitu ambavyo hakuwahi kuvikubali ni pamoja na matumizi ya njia ya uzazi wa mpango, akiamini kuwa vingeweza kumletea madhara ya kiafya.

Katika watoto hao 15, Neema hakuwahi kuzaa mapacha wala kuzaa kwa njia ya oparesheni badala yake alikuwa akizaa kwa njia ya kawaida tena baadhi ya watoto akizalia nyumbani.

Mwananchi ilimfahamu mwanamke huyo ambaye kwa sasa ni marehemu na kurusha changamoto za malezi alizokuwa alikutana nazo kupitia mitandao ya kijamii ya Mwananchi, ambapo baadhi ya wadau waliguswa na kuisaidia familia hiyo.

Hata hivyo kwa mujibu wa mume wake amedai kuwa miezi miwili iliyopita, mke wake huyo alianza kuumwa na akapelekwa hospitali na kupata matibabu ambayo yalimpa nafuu na hivyo kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Mume huyo anasema wiki mbili zilizopita mke wake alianza kuumwa tena na kurudishwa hospitali hata hivyo hali ilizidi kuwa mbaya na ndipo alipoamua kumuachisha ziwa mtoto wake mdogo na ilipofika Novemba 16 alizidiwa na kufariki dunia.

Related Posts