Waziri Chana kwenye mkutano mkubwa wa kimataifa Arusha,atoa mikakati hii

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana amesisitiza umuhimu wa kuwa na mikakati endelevu katika kukuza Sekta ya Utalii na Ukarimu hususan katika nyanja za utunzaji wa mazingira, ustawi wa jamii, kutumia teknolojia za kidijitali na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa maendeleo endelevu na ustawi wa Sekta ya Utalii.

Ameyasema hayo leo Novemba 21, 2024 wakati akifungua rasmi Mkutano wa tatu wa Kimataifa wa Kuunganisha wanataaluma na wadau wa Utalii na Ukarimu katika Nchi Zinazoendelea uliofanyika jijini Arusha.

“Mkutano huu una lengo la kuunganisha wanataaluma na wadau wa sekta ya utalii ambapo kupitia mkutano huu wanataaluma watatoa matokeo ya tafiti na mifumo ya kinadharia inayohitajika kuelewa changamoto kubwa zilizopo, wakati wadau wa sekta watatoa ufahamu wa vitendo kupitia uzoefu wao katika kazi na biashara za utalii ili kusaidia kuleta uvumbuzi, kuimarisha mafunzo, na kuongeza ajira” amesema Mhe. Chana.

Amefafanua kuwa ili Sekta ya Utalii na Ukarimu iendelee ni vyema kukawa na hatua za kulinda mazingira kwa kuhifadhi misitu, wanyamapori, na rasilimali za baharini pamoja na kuwepo na ushirikishwaji wa jamii kwa kuwepo na utalii wa kijamii.

Kuhusu matumizi ya teknolojia ya kidijitali, Mhe. Chana amefafanua kuwa msisitizo juu ya teknolojia katika mkutano huo ni muhimu hasa katika kujadili mada za Mawasiliano ya kidigitali na matumizi ya kompyuta katika Ukarimu na Utalii akitolea mfano kutalii kidigitali na kuwa na vyumba vya hoteli vinavyoendeshwa kidigitali.

Aidha, amesema mabadiliko ya Tabianchi na Maendeleo ya Utalii yanapelekea kufikiria upya kuwa, utalii sio tu njia ya kufikia malengo bali unaambatana na utunzaji wa mazingira na uboreshaji wa jamii.

“Mijadala kuhusu kupunguza athari za mazingira katika Ukarimu na Utalii pia usimamizi wa taka katika upande wa Ukarimu, zinatoa changamoto ya kufikiria upya namna ilivyofanyiwa kazi na kuhakikisha kwamba Tanzania inapata namna nzuri endelevu itakayosaidia sekta ya Utalii kukua.

Related Posts