Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa, amesema licha ya kufungua milango ya ushirikiano kwa Wadau wa Sekta ya Habari kuifikia ofisi yake wakati wowote, anawaalika kuwa tayari kusema, kusikia, na kukubaliana na hali halisi.
Waziri Silaa alitoa kauli hiyo leo, tarehe 21 Novemba 2024, wakati wa kikao cha kwanza cha kufahamiana na Wajumbe wa Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) kilichofanyika Ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), jijini Dar es Salaam.
“Milango iko wazi wakati wote, mnaweza kufika ofisini kwangu… ili tuweze kutengeneza mazingira ya kukutana, kujadiliana, kushauriana na kuona wizara hii ni Wizara yenu. Kikubwa ni kuwa na mtazamo wazi; wakati wote mnapofika, muwe tayari kusema, muwe tayari kusikia, na vilevile muwe tayari kukubaliana na hali halisi,” alisisitiza Waziri Silaa.
Amesema malengo ya kufungua milango kwa wadau wa Habari na kwa waandishi wa Habari mmoja mmoja ni kuijenga na kuikuza tasnia ya Habari nchini.
Aidha, Waziri Silaa aliahidi kuendelea kufuata maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha tasnia ya Habari inakuwa huru, inafanya kazi kwa utaratibu utakaowasaidia waandishi kutekeleza majukumu yao, kuwapa haki Watanzania kupata taarifa, na kutimiza wajibu wao.
Hata hivyo, Waziri Silaa alikumbusha wadau wa Habari kwamba maono ya Rais Samia ya kutaka uhuru wa Habari lazima yaendane na wajibu. Alifafanua kwamba msamaha alioutoa wa kuvifungulia vyombo vya Habari vilivyofungiwa haimaanishi vyombo hivyo havikufanya makosa.
“Kama mnavyokumbuka, Mheshimiwa Rais wiki mbili tu baada ya kuingia madarakani, alizifungulia Online TV zote ambazo zilikuwa zimefungiwa, akavirudishia leseni vyombo vya Habari vilivyokuwa vimefungiwa,” alisema Waziri Silaa, na kuongeza:
“Vyombo vya Habari vilivyofungiwa, siyo kwamba havikufanya makosa, hapana. Kisheria vilifanya makosa, lakini kwa mapenzi yake, busara zake, na ustahimilivu wake, na hata mlioona alifanya katika sekta nyingine, ikiwemo 4R zake, aliona ni vema kila mtu akapata fursa ya kufanya kazi… kwa sababu Online Media inatoa ajira kwa vijana wengi sasa.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CoRI, Bw. Ernest Sungura, ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), alisema anaamini kikao hicho cha kufahamiana na Waziri Silaa kitafungua fursa ya vikao kazi zaidi vitakavyotumika kuwasilisha hoja nyingine za kuzifanyia kazi.