Zanzibar yazidi kufunguka kwa uwekezaji

Unguja. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff amesema Zanzibar inazidi kufunguka na uwekezaji kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Amesema kwa kipindi cha miaka minne kuna miradi zaidi ya 390 ya uwekezaji ambayo imesajiliwa Zanzibar sawa na ongezeko la asilimia 200 ikilinganishwa na kipindi cha nyuma ambacho ilikuwa ikisajili miradi takribani 50 kwa mwaka.

Miradi iliyowekezwa amesema ina thamani ya Dola 5.5 bilioni za Marekani ambazo zimeingia kwenye uchumi wa Zanzibar.

Ametoa kauli hiyo jana Novemba 20, 2024 alipozindua toleo la tatu la jarida la uwekezaji Zanzibar (ZIBI) ambalo linaelezea masuala ya uwekezaji na fursa zilizopo katika kisiwa hicho.

“Maono ya Rais Dk Hussein Mwinyi, dhana ya kukodisha visiwa imeleta tija kubwa sana, ukienda maeneo huru ya visiwani Pemba yameboreshwa, na kwa sasa kuna miradi mikubwa sita inakuja katika maeneo hayo, kwa hiyo kwetu sisi kiuwekezaji tumefunguka na jitihada za Serikali zimeleta matunda,” amesema.

Shariff amesema Serikali imeweka sheria ambazo ni rafiki zaidi za kuleta wawekezaji wa hali ya juu badala ya uwekezaji mdogo mdogo.

Hata hivyo, amesema wanapokea baadhi ya changamoto ikiwemo kuendelea kuweka sera na sheria nzuri na kuendelea kufungua milango zaidi, akizitaka sekta binafsi kujitayarisha kuwa na uwezo wa kifedha katika ubunifu wa kibiashara na uwekezaji.

“Kwetu sisi ni somo tumelipata kuwa tunajipangaje kuziba haya mapengo ili Zanzibar ije juu katika suala la biashara,” amesema.

Kuhusu ZIBI, Shariff amesema jarida hilo limebeba mambo mengi kuhusu uchumi wa buluu, utalii, biashara, teknolojia na miundombinu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mwanana Communications, Hissham Abdukadir amesema kuna mahitaji makubwa ya taarifa za biashara na uchumi Zanzibar kwa sababu kabla ya kuanzishwa kwa jarida hilo hakukuwa na chapisho linalozungumzia biashara, uchumi na uwekezaji, kwa hiyo ni fursa.

Waziri mstaafu wa Nishati, Mafuta na Gesi wa Oman, Dk Mohammed Al Rumhy amesema Zanzibar ni sehemu nzuri ya kuwekeza, hivyo wawekezaji wakija wanajihisi wapo salama na upendo mkubwa wa wananchi wa kisiwa hicho.

“Ni matumani yangu kuwa Zanzibar inaweza kuwa katika nafasi nzuri ya uwekezaji duniani,” amesema.

Meneja Utalii katika Taasisi ya Rais ya Kufuatilia Utendaji Serikalini (PDB), Hafsa Mbamba amesema kupitia sera nzuri, ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi utapaisha uwekezaji.

Mwekezaji, Max Maxwell amesema fursa zipo Zanzibar lakini bado kunahitajika kuendelea kuimarishwa zaidi miundombinu.

Related Posts