Unguja. Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imefanya marekebisho madogo ya mipaka ya majimbo ya Wete na Mtambwe kiswani Pemba.
Hatua hiyo imetokana na mabadiliko ya mipaka ya wadi ya Piki yaliyofanywa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi amesema hayo leo Novemba 21, 2024 kwamba mabadiliko hayo ya mipaka ya majimbo yanahusisha Shehia ya Limbani iliyokuwa katika wadi hiyo katika Jimbo la Wete na Shehia ya Mzambarautakao katika Jimbo la Mtambwe, yalitangazwa katika gazeti la Serikali Agosti 28, 2020 kwa tangazo namba 108 la mwaka 2020.
“Shehia ya Limbani awali ilikuwa katika Wadi ya Piki jimbo la Mtambwe na kwa sasa itasomeka ni Shehia ya Limbani katika Wadi ya Jadida, Jimbo la Wete.
Shehia ya Mzambarautakao katika Wadi ya Pandani, Jimbo la Pandani itasomeka katika Wadi ya Piki jimbo la Mtambwe.
Hata hivyo, amesema katika kueleka Uchaguzi Mkuu mwaka 2025, ZEC haitachunguza idadi ya mipaka na majina ya majimbo, badala yake yatabaki kama ilivyokuwa katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.
Katika hatua nyingine, Jaji Kazi amesema ZEC inatarajia kuendesha awamu ya pili ya uandikishaji wapigakura Februari mosi 2025 kuanzia Wilaya ya Micheweni, Pemba na kumalizia Wilaya ya Mjini, Machi 17, 2025.
Amesema uandikishaji huo utafanyika katika vituo 407 kwa muda wa siku tatu kwa kila shehia, Unguja na Pemba.
Kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 wapigakura wapya 78,922 waliotimiza miaka 18 na watakaotimiza umri huo wanatarajiwa kuandikishwa kabla ya tarehe ya uchaguzi.
Amesema pamoja na uandikishaji huo, ofisi za wilaya za Tume hiyo zinaendelea kutoa huduma kwa kuhamisha taarifa za wapigakura, kusahihisha taarifa za wapigakura, na kupokea maombi ya kufuta taarifa za wapigakura waliokosa sifa.
Amewataka wananchi wenye sifa kujitokeza kujiandikisha wakati ukifika ili kushiriki uchaguzi mkuu ujao.
Mkurugenzi wa ZEC, Idarous Faina amesema wamejipanga kuhakikisha kila anayestahili kuandikwa anaandikishwa na kushughulikia changamoto zote zinazojitokeza.
ZEC iliandikisha wapigakura wapya awamu ya kwanza Desemba 2, 2023 hadi Januari 15, 2024 ambapo wapigakura wapya 57,883 waliandikishwa Unguja na Pemba.