AKILI ZA KIJIWENI: Makocha wageni kimewakuta Ligi Kuu

KIJIWE kimeanza taratibu kuwakataa makocha wa kigeni wanaofundisha timu zetu za Ligi Kuu msimu huu.

Zamani kiliwapa sana dhamana na kuwamwagia ujiko wa kutosha mbele ya makocha wazawa lakini sasa hivi bwana hapa kijiweni tumeamua kuwageuzia kibao.

Huu muendelezo wa makocha wa kigeni kutimuliwa kwa idadi kubwa kulinganisha na wazawa kabla hata Ligi haijafika nusu msimu unatufanya tuone kuwa hakuna haja kwa timu nyingi kuchukua hao wageni.

Kuondolewa kwao wengi kunafanya tuamini wana mapungufu ya kiufundi hata ya nje ya uwanja ambayo yanafanya timu kuachana nao.

Msimu kabla haujaanza, Coastal Union ilianzisha nuksi kwa makocha wa kigeni hapa nchini msimu huu baada ya kumtimua David Ouma na baadaye akafuatiwa Yousouph Dabo wa Azam kisha ikaja zamu ya mzawa Fikiri Elias ambaye yeye aliamua kujiweka kando.

Baadaye akaondolewa Goran Kopunovic wa Pamba, mwingine akawa ni Paul Nkata wa Kagera Sugar, akaja Mwinyi Zahera wa Namungo na baadaye Francis Kimanzi wa Tabora United akafuata nyayo.

Kabla mambo hayapoa, tukashuhudia Miguel Gamondi wa Yanga akivunjiwa mkataba wake na pia hapohapo tukasikia kocha wa KMC, Abdihamid Moalin akiachana na klabu hiyo kisha kutimkia Yanga ambako anaenda kuwa mkurugenzi wa ufundi.

Wakati hayo yakitokea, makocha wazawa wengi tu wanapeta kwenye timu zao na viongozi wanaonyesha imani kubwa nao huku baadhi timu zao zikionyesha ushindani wa hali ya juu kwenye ligi.

Labda viongozi wanaona wanachoka kutumia gharama kubwa kuwa na makocha wa kigeni ambao bado hawazipi timu zao kitu cha tofauti na kile wanachokipata kutoka kwa wazawa.

Related Posts