Athari za unyanyasaji kwa mjamzito na mtoto atakayezaliwa

Dar es Salaam. Katika kuelekea siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, jarida hili linaangazia athari za kiafya kwa mjamzito aliyepitia na anayepitia unyanyasaji wa kijinsia kwa mwenza wake pamoja na wale wanaobakwa au mimba kukataliwa.

Unyanyasaji wa kijinsia (GBV) unarejelea vitisho au vitendo vyenye madhara vinavyoelekezwa kwa mtu binafsi au kikundi kulingana na jinsia yao, kimataifa siku hizo huanzia Novemba 25 hadi Desemba 10.

Ujauzito mara nyingi huchukuliwa kuwa tukio la kuleta maisha, linalojawa na matarajio na ndoto za baadaye, huku mama ndiye anayemkuza mtoto tumboni kwa miezi tisa, kipindi muhimu kinachoamua uimara wa mtoto kiafya.

Hata hivyo, kwa wasichana wadogo na wanawake waliopata ujauzito kutokana na kubakwa, tukio hili hugeuka kuwa jaribu lenye kuogofya ambalo linawafunga katika mtandao tata wa msongo wa mawazo, aibu na unyanyapaa.

Kwa kutokujua, baadhi ya waume huendeleza unyanyasaji kwa wake zao katika kipindi hiki, bila wao kujua hujikuta wanaharibu afya za watoto wao watakaozaliwa.

Akizungumza na jarida hili, Mtaalamu wa Saikolojia na Mhadhiri Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS), Faithness Kiondo anasema hali hiyo humfanya mama kuzalisha homoni ya msongo ambayo huenda moja kwa moja kuharibu makuzi na ubongo wa mtoto.

“Kuna tafiti zinasema mama mjamzito akiwa na sonona anarithisha mtoto, zile gene au vinasaba vya sonona, akizaliwa tu wakati wowote kitu kidogo sana ambacho kingeweza kumalizwa taratibu kitampeleka yule mtoto kwenye sonona baadaye,” anasema Faithness.

Anasema kutokana na hali hiyo, tangu akiwa tumboni ubongo unaharibika, kwa hiyo anaendelea na zile athari za toka tumboni mpaka anapozaliwa.

Faithness anataja athari hizo kuwa ni pamoja na mtoto kuchelewa katika hatua za ukuaji, kuwa na akili ya taratibu, kuwa na tabia za ugomvi, utundu kupitiliza, ujeuri, viwango vya juu vya wasiwasi, woga na mashaka pamoja woga katika kushughulikia changamoto za kimaisha.

Takwimu zinaonyesha kesi 29,373 ziliripotiwa polisi mwaka 2021, huku kesi 6,305 sawa na asilimia 21.5 zilikuwa za kubakwa na asilimia 19.5 sawa na watu 5,751 na wanawake 20 walipata mimba za maharimu.

Mpaka Machi 2022 kutoka 2019 kesi 19,726 walibakwa na GBV zilikuwa 27,838 na vichanga 443 vilitupwa.

Faithness anasema wengi hufikia hatua ya kutupa vichanga kwa kuona mimba kama matokeo ya ubakaji. “Unakuta wabakaji ni wale walioaminiwa, wakiwemo baba, kaka, mjomba, baba mdogo, kaka na wengine wa karibu.”

Ubakaji unapotokea ndani ya ndoa, familia na watu walioaminika, athari za kisaikolojia huwa za kuumiza sana mjamzito na zinaweza kuwa na madhara ya muda mrefu yanayozidi muda wa tukio lenyewe.

“Inafika mahali ambapo baadhi ya wasichana hawa hujaribu kujiua, wengine hufaulu na wengine hushindwa. Sasa unaweza kuwazia hali yao ya kiakili wanaposhindwa,” anasema Faithness.

Anasema msichana aliyebakwa hukumbwa na msongo wa akili na hali huwa mbaya zaidi pale msichana huyo anapogundua kuwa ni mjamzito.

Faithness anasisitiza umuhimu mkubwa wa wasichana waliobakwa kupokea ushauri wa kina, kwani wanapofika hospitalini mara nyingi hupewa tu dawa za matibabu.

Anasema ushauri wa kisaikolojia unachukua nafasi muhimu katika mchakato wa uponyaji kwa waathirika wa ubakaji, kama ilivyo kwa manusura wa ukatili wa kijinsia popote pale.

“Athari za ukatili wa kijinsia kwa waathirika ni kubwa na ushauri wa kisaikolojia hutoa msaada wa msingi unaoshughulikia athari za muda mfupi na mrefu za kisaikolojia, kihisia na kijamii za trauma hiyo,” anasema.

“Ubakaji mara nyingi husababisha athari mbalimbali za kisaikolojia, ikiwa ni pamoja na wasiwasi, mfadhaiko, aibu, hasira, matatizo ya kisaikolojia yanayosababishwa na kiwewe (PTSD) na hali ya kukata tamaa. Ushauri husaidia waathirika kushughulikia hisia hizi nzito na kupitia maumivu yao katika mazingira salama na yenye msaada,” anasema Faithness.

Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi, Elias Kweyamba anasema mtoto anayezaliwa na mama aliyekuwa na msongo wa mawazo anaweza kupata baadhi ya tabia na changamoto mbalimbali.

Anasema mtoto anaweza kuonyesha tabia kama vile ugomvi, ujeuri, hasira za ghafla au kupoteza uwezo wa kujidhibiti na hiyo inaweza kuanza utotoni na kuendelea kadiri anavyokua.

Pia anasema msongo wa mawazo wa mama unaweza kusababisha watoto kuwa na viwango vya juu vya wasiwasi, woga au mashaka.

“Mtoto wa aina hii anakuwa na hali ya kutotulia au woga wa kushughulika na changamoto za maisha, na hii kama hatapata tiba mapema inaweza kwenda hadi anapokuwa mtu mzima,” anasema Kweyamba.

Anabainisha kuwa mtoto anayezaliwa katika hali hiyo anaweza kukosa usingizi mzuri au kuwa na usingizi wa mara kwa mara usio tulivu, hali inayoweza kuathiri ukuaji wake wa kiakili na kimwili.

Dk Kweyamba anasema msongo wa mawazo wa mama unaweza kuathiri uwezo wa mtoto kujifunza au kumudu masomo shuleni na anaweza kuwa na matatizo ya kumbukumbu, umakini au uwezo wa kushughulikia taarifa mpya.

“Baadhi wanaweza kuwa na hali ya huzuni na sonona katika umri mdogo kutokana na athari za homoni za msongo walizoathiriwa nazo wakati wa ujauzito.

“Pamoja na hayo, watoto wanaweza kuwa na matatizo ya kuwasiliana au kushirikiana vizuri na wenzao. Wanakuwa na hali ya kutokujiamini, kuepuka mawasiliano au hata kushindwa kuunda uhusiano mzuri na watu wa karibu,” anasema.

Utafiti unaonyesha kuwa manusura wa ukatili wa kijinsia mara nyingi hukumbwa na changamoto zinazoathiri uwezo wao wa kushughulikia kiwewe ‘Post traumatic stress disorder’, hali inayozidishwa zaidi pale mkosaji ni mwanafamilia, mtu ambaye kawaida huhusishwa na usalama na upendo.

Naomi Jones (39) ni miongoni mwa wanawake waliopitia ukatili akiwa katika ndoa, anasema nyakati zote akiwa mjamzito alikuwa hatamani kukutana na mumewe.

“Mtalaka wangu alikuwa mkali sana, sikukwazana naye isipokuwa kipindi cha ujauzito nilikuwa sipendi kabisa kukutana naye, alichokifanya mume wangu alikuwa akinibaka karibu kila siku nikiwa na mimba, nilivumilia ila ilikuwa inaniumiza,” anasimulia Naomi, mama wa watoto watatu wa kiume.

Anasema kutokana na hali hiyo, presha ilikuwa ikipanda mara kwa mara akiwa mjamzito, ingawaje baadaye alikuja kuachana na mumewe.

“Inaweza kusemekana ni kurithi tabia za baba yao, lakini kwa kuwa mimi nimesoma nimebaini kuwa hali yangu ya msongo wakati wa ujauzito ndiyo imeleta hatima ya tabia za watoto wangu, ingawa shangazi zao wanasema watoto wamerithi tabia ya ukali kutoka kwa baba yao.

“Lakini kwa kuwa baba mkwe wangu alikuwa mkali zaidi ya mume wangu, hii siyo tabia ya kurithi, huenda mama mkwe wangu naye alipitia hali fulani isiyo sawa kipindi amebeba ujauzito wa mume wangu,” anasema naomi.

Mwanamke mwingine (hakutaka kutaja jina) ambaye ni manusura wa ubakaji uliofanywa na mwanafamilia wa karibu, anasema kuwa wasichana wadogo mara nyingi hujilaumu na kuhisi aibu, wakiamini kimakosa kwamba walihusika kwa namna fulani katika shambulio hilo.

“Mgongano huu wa ndani unakuwa mkubwa zaidi pale ujauzito unapotokea, kama ilivyotokea kwangu, kwa kuwa jamii mara nyingi huweka unyanyapaa kwa wale wanaobeba mzigo wa asili hiyo, ghafla nilijikuta naporomoka katika hali ya kujiamini na utambulisho wangu,” anasema.

Anasema mabinti wengi wadogo hujifunza kuficha ukatili wa kijinsia, jambo linalozidisha hisia zao za kuwa wamekwama na uwezekano wa unyanyapaa huwazuia kutafuta msaada au kuripoti uhalifu huo.

Mwanamke huyo anasema athari za kisaikolojia za kubeba mtoto aliyezaliwa kutokana na ubakaji wa kifamilia zimesambaa hadi utu uzima wake, zikiathiri mahusiano yake ya baadaye na uwezo wake wa kuunda mahusiano yenye afya.

Anakiri kuwa matatizo ya kuamini watu, hofu ya ukaribu wa kimapenzi na changamoto za kudhibiti hisia ni mambo ya kawaida miongoni mwa wale ambao hawajapata msaada wa kutosha wa kisaikolojia.

Mwanamke huyo anasema kwa wengi, kiwewe hicho huwa ni lenzi wanayotumia kutazama dunia, hali inayosababisha changamoto za kudumu za mahusiano.

“Nina msongo wa mawazo, sonona na hofu. Lakini nilibakwa na kupata trauma, lakini baadaye nikajigundua kuwa na ujauzito na mpaka sasa kila nikimuona mtoto wangu nakumbuka kubakwa, maisha yangu yote natembea na ushahidi,” anasimulia mwanamke huyo.

Related Posts