Benki ya NBC yatambulisha kampeni ya Kilimo Mahususi kwa wakulima na wafugaji Mbeya

 

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC), imetambulisha kampeni yake ya ‘Shinda Mechi Zako Kinamna Yako na NBC Shambani’ kwa wakulima na wafugaji wa wilaya za Rungwe na Kyela mkoani Mbeya ikiwa ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo kuchochea kasi ya ukuaji wa sekta za kilimo na ufugaji nchini kupitia uchumi jumuishi unaochagizwa na huduma rasmi za kifedha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kyela, Mbeya … (endelea).

Hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo imefanyika mapema leo Tukuyu, wilayani Rungwe ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Jaffar Haniu, huku pia ikihushisha uwepo wa wadau mbalimbali wa sekta za kilimo na ufugaji kutoka wilaya hizo mbili wakiwemo viongozi wa vyama vya msingi na vyama vikuu vya ushirika vya wakulima na wafugaji (AMCOS), pamoja na wadau wengine wanaoshiriki kwenye mnyororo wa thamani wa sekta hizo.

Meneja wa NBC Tawi la Tukuyu, Erick Mbeyale aliwaongoza maofisa wengine wa benki hiyo kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo inayotoa fursa kwa wakulima na wafugaji wa wilaya za Rungwe na Kyela mkoani Mbeya kushinda zawadi mbalimbali ikiwemo Simu janja, pikipiki na mizani za kisasa kwa ajili ya kupimia mazao yao.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Haniu pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa jitihada zake endelevu zinazolenga kuwasaidia wakulima na wafugaji alisema ujio wa kampeni hiyo kwenye wilaya za Rungwe na Kyela utasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi wa wadau mbalimbali wa sekta hizo hususani kupitia huduma mbalimbali za kibenki zilizobuniwa mahususi kwa makundi hayo ikiwemo mikopo rafiki.

“Ubora zaidi wa kampeni hii unaonekana pale inapohusisha utoaji wa elimu ya nidhamu ya fedha miongoni mwa wakulima mmoja mmoja na vyama vya ushirika hatua ambayo itawajengea uwezo wa kuona umuhimu wa kujiwekea akiba, umuhimu wa kutumia bima mbalimbali ikiwemo bima ya afya, bima za kilimo pamoja na kuwekeza kwenye zana za kisasa za kilimo.’’

“Hatua hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuhamasisha wakulima wetu kugeukia huduma rasmi za kifedha na hivyo kuchochea uchumi jumuishi. Hii ni hatua kubwa sana ikilinganishwa na tulipotoka miaka kadhaa iliyopita ambapo wakulima na wafugaji walikuwa hawaaminiki na taasisi za kifedha kutokana na kutokuwa waaminifu na wengine kutokuwa na dhamana,’’ aliongeza.

Akifafanua zaidi kuhusu kampeni hiyo, Meneja wa NBC Tawi la Tukuyu, Erick Mbeyale alisema walengwa wa kampeni hiyo ni wakulima, wafugaji na vyama vya msingi vya wakulinma na wafugaji ambao wanahudumiwa na benki hiyo.

Kwa mujibu wa Bw Mbeyale, ili mkulima au mfugaji mmoja mmoja ashinde zawadi hizo anatakiwa kwenye akaunti yake awe na fedha kuanzia Sh. 500,000 mpaka 3,500,000 na kwamba kwa AMCOS inatakiwa kuwa na kati ya Sh. Milioni 50 hadi Milioni 100.

“Lengo la kampeni hii ni kuwahamasisha wakulima na wafugaji kutunza fedha zao kwenye mifumo rasmi ya kifedha hasa benki badala ya kutunza kwenye mifumo isiyo rasmi,’’ alisema.

Awali akiwasilisha mada kuhusu matumizi ya bima mbalimbali zinazotolewa kwa wakulima na wafugaji kupitia benki hiyo, Meneja Uhusiano Kitengo cha Bima wa Benki ya NBC Kanda ya Kusini, Amani Swilla alisema kupitia huduma hiyo, wakulima na wafugaji wapo kwenye nafasi ya kunufaika kupitia bima za afya, bima ya mazao pamoja na bima za vyombo vya moto.

“Kupitia huduma hii muhimu ya bima wakulima na wafugaji wanaweza kusaidiwa kupitia fidia pale mazao yao yanapokumbwa na majanga ya asili ikiwemo mvua ya mawe, mafuriko, majanga ya moto, na majanga mengine ya asili,’’ alitaja.

About The Author

Related Posts