UTAMU wa Ligi ya Championship unaendelea kushika kasi, ukiingia raundi ya 10 na baada ya jana kuchezwa mechi mbili, kesho zitapigwa mbili kwenye mwendelezo wa kuwania kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Mchezo wa mapema utapigwa saa 8:00 mchana na TMA iliyoichapa Cosmopolitan mabao 2-1, itakuwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha dhidi ya Mtibwa Sugar iliyotoka sare ya mabao 2-2, mechi ya mwisho na Biashara United.
Kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume Mara, Biashara United itacheza na Songea United iliyoifunga bao 1-0 Kiluvya United huku, African Sports iliyochapwa mabao 2-1 na Stand United itaikaribisha Mbuni iliyoshinda 3-0, dhidi ya Green Warriors.
Ligi hiyo itaendelea tena keshokutwa Jumapili kwa michezo mitatu kupigwa na saa 8:00 mchana, Stand United itakuwa kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga kucheza na Mbeya City yenye kumbukumbu nzuri baada ya kuifunga Transit Camp kwa mabao 2-1.
Saa 10:00 jioni, Cosmopolitan itakuwa kwenye Uwanja wa Mabatini kuikaribisha Geita Gold iliyoichapa Bigman FC bao 1-0, huku Polisi Tanzania iliyotoka sare ya 1-1 na Mbeya Kwanza itacheza na Green Warriors kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi.
Akizungumzia mwenendo wa Ligi hiyo, Kocha wa Biashara United, Mussa Rashid alisema hadi sasa hakuna timu yenye uhakika wa kupanda moja kwa moja kutokana na gepu la pointi lililopo, hivyo muhimu kwao ni kuhakikisha wanapata matokeo chanya.
“Ukiangalia timu zilizopo juu na zile za chini utaona hakuna tofauti kubwa sana, ni mapema kusema kuna mwenye uhakika wa kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao, ndiyo maana kila mchezo unauona ni mgumu bila ya kujali unacheza nyumbani au ugenini.”