Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, amekitaka Chuo cha Kodi nchini kuhakikisha kinatoa mafunzo kwa wanafunzi yatakayowajengea uwezo wa kujiajiri, kuwa na ufanisi mkubwa kazini na kubuni njia rahisi za ulipaji kodi.
Aidha, ametoa wito kwa chuo hicho kutoa mafunzo si tu kwa wanafunzi wake, bali pia kwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Watanzania kwa ujumla, ili kuongeza idadi ya wataalamu waliobobea katika ukusanyaji wa kodi.
Mwandumbya ametoa maagizo hayo leo, Novemba 22, 2024, jijini Dar es Salaam wakati wa Mahafali ya 17 ya chuo hicho, akisisitiza mchango mkubwa wa chuo hicho katika kuboresha utendaji wa TRA.
“Serikali inatambua mchango mkubwa wa Chuo cha Kodi katika kutoa mafunzo kwa watumishi wa TRA na Watanzania ili kuongeza makusanyo ya kodi… Niwasihi mwendelee kutoa mafunzo yenye viwango vya hali ya juu, kwa kuzingatia maendeleo ya sayansi na teknolojia ambayo ni nyenzo muhimu katika ufundishaji duniani ya sasa,” amesema Mwandumbya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TRA, Uledi Mussa, amesisitiza jukumu la wahitimu hao kutumia maarifa yao kuhamasisha ulipaji kodi nchini.
“Nyinyi ni mabalozi wa TRA. Nitashangaa kama hamtakuwa wa kwanza kutoa elimu ya kodi na kudai risiti. Mmetokea chuo hiki, na tutakapotangaza ajira, wahitimu wa mwaka huu tutawapa kipaumbele. Msiache kuomba nafasi hizo,” amesema Mussa.
Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Isaya Jairo, amesema chuo hicho kinaendelea kuboresha utoaji wa elimu kwa njia za kisasa za kidijitali, huku maandalizi ya utoaji wa mafunzo ya masafa kwa njia ya mtandao yakiwa yamepiga hatua kubwa.
“Tunatarajia mafunzo ya elimu masafa yatakapoanza yataongeza idadi ya wanafunzi wanaopata mafunzo chuoni hapa na yatasaidia kuwafikia wanafunzi wengi kwa urahisi, wakati mmoja na kwa gharama nafuu, hivyo kuongeza idadi ya wahitimu,” amesema Profesa Jairo.
Ameongeza kuwa mafunzo yanayotolewa chuoni hapo yanazingatia mabadiliko ya sayansi, teknolojia na uchumi, ili kukidhi mahitaji ya soko la wataalamu katika sekta za forodha na kodi nchini.