Mkuu wa Wilaya ya Mkingq Gilbert Kalima akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma ya kufanya uwekaji wa miundombinu ya umeme katika nyumba wilayani humo kutoka kwa mafundi wa VETA wa wilaya hiyo.
Mkuu wa Chuo cha VETA Wilaya ya Mkinga, Calvin Haule akizungumza kuhusiana na mafundi wa umeme wa VETA kutoa huduma bure.
Baadhi ya huduma ya bure ya mafundi umeme katika nyumba wilayani Mkinga.
Na Mwandishi Wetu
CHUO cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Mkinga, Mkoani Tanga kimeanza kutoa bure huduma ya ufundi umeme wa majumbani (wiring) kwa kaya 50 zenye kipato cha chini katika Tarafa mbili wilayani humo.
akizungumza jana tarehe 21 novemba, 2024, wilayani mkinga wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo, mkuu wa wilaya ya mkinga, mhe. gilbert kalima, amepongeza mpango huo na kusema kuwa chuo hicho kimeonesha umuhimu wake kwa jamii ya mkinga.
amesema ubunifu huo ni sehemu ya kurudisha kwa jamii na kuonesha tija waliyoipata vijana wanaosoma chuoni hapo.
Sambamba na hilo, Kalima amesema chuo hicho pia kimesaidia kwa kiasi kikubwa kuzalisha mafundi wenye ujuzi, wengi wao wakiwa kutoka wilaya ya Mkinga, hivyo kupunguza changamoto ya upatikanaji wa mafundi umeme wilayani humo.
“Kwa muda mrefu, mafundi umeme wengi waliokuwa wakifanya kazi wilayani Mkinga walikuwa wakitoka Tanga mjini na baadhi yao kutoka nje ya mkoa wa Tanga, na tatizo kubwa lilikuwa ni kukosa uaminifu na baadhi yao kudhulumu wananchi. Lakini sasa, kupitia chuo cha VETA, tunapata mafundi waliopata mafunzo bora na wanaoweza kutoa huduma kwa ufanisi,” amesema Mhe. Kalima.
Ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanapeleka vijana wao katika chuo hicho ili waweze kupata ujuzi mbalimbali kupitia kozi zinazotolewa, ambazo ni za muda mrefu na mfupi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha VETA Wilaya ya Mkinga, Calvin Haule, amesema kuwa mpango huo unalenga kusogeza huduma ya umeme kwa jamii na kupunguza gharama ya kulipa mafundi kutoka maeneo ya mbali.
Haule ameongeza kuwa mpango huo pia utawawezesha wanafunzi kujiimarisha kwenye mafunzo kwa vitendo na kwamba huduma hiyo itasaidia kaya kuboresha maisha yao na kukuza shughuli za kiuchumi zinazotokana na nishati ya umeme.
Matukio katika picha katika hafla ya uzinduzi mafundi umeme kufunga bure