Dar es Salaam. Wakati maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yakitarajiwa kufanyika kwa ngazi ya taifa Machi 2025, Serikali imesema hatua hiyo itakuwa fursa ya kutathmini hatua iliyofikiwa na wanawake katika ujenzi wa taifa.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalum, Dk Dorothy Gwajima ameyasema hayo leo Novemba 22, 2024 jijini Dar es Salaam kwenye uzinduzi wa kamati ya kitaifa ya maandalizi maadhimisho hayo yenye wajumbe 26.
Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa Machi 8 kila mwaka kwa namna mbalimbali, lakini mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika kitaifa.
Dk Gwajima amesema tathmini itakayofanyika juu ya hatua iliyofikiwa na mwananamke, isijiegemeze kwa wale maarufu pekee, iwaangazie na wengine walioko katika mitaa na kata, ambao wanafanya vizuri katika nyanja za biashara, elimu, siasa na nyinginezo.
“Huko mitaani kuna wanawake wanafanya vizuri huko, tukawaibue wajulikane na hata kufahamu changamoto zao kupitia jukwaa hilo,”ameeleza.
Ameeleza kuwa maadhimisho hayo ni fursa ya kuwakutanisha wadau mbalimbali wa uwezeshaji wanawake kujadili hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mikakati ya kuwainua.
Mikakati hiyo ni ile ya kitaifa pamoja na kimataifa ili wananchi wawe na uelewa wa nini kinaendelea katika kuhakikisha maisha ya mwanamke yanaboreshwa.
“Ni vyema pia kutoa elimu kwa wananchi hadi vijijini ili waweze kujua mambo yanayofanyika katika kuwezesha wanawake, nafasi na wajibu wao katika utekelezaji wake,” amesema.
Waziri huyo amesema kwa hapa nchini maadhimisho hayo hufanyika kwa ngazi ya kitaifa kila inapofika miaka mitano na mara ya mwisho yalifanyika 2020 mkoani Simiyu.
“Utaratibu huo uliowekwa na nchi ulilenga kutoa fursa kwa wananchi wote kuanzia ngazi za mitaa kushiriki ili kuimarisha shughuli za maendeleo, haswa zinazofanywa na wanawake katika sekta mbalimbali,” amesema.
Kwa upande wake Maida Waziri ambaye ni Rais wa Sauti ya Wajasiriamali Tanzania na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, amesema jukwaa hilo pia ni fursa ya kuwatambua watu mbalimbali ambao wamekuwa wakipigania haki na ustawi wa wanawake.
Pia kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika masuala ya maendeleo ili kufikia usawa wa kijinsia katika sekta mbalimbali.