Kiama matapeli mtandaoni chaja | Mwananchi

Dar es Salaam. Katika kukabiliana na wimbi la uhalifu wa utapeli mtandaoni, Serikali imeunda kikosi kazi kitakachotafuta mbinu mahususi za kukabiliana nao.

Kuundwa kwa kikosi kazi hicho ni mojawapo ya maazimio ya kikao kilichowakutanisha mawaziri wa Mambo ya Ndani na Wizara ya Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na wadau wanaohusika na sekta za mawasiliano, usalama na fedha.

Hatua hiyo imefikiwa wakati ambao yamekuwapo matukio kadhaa ya uhalifu mtandaoni ambayo yameripotiwa, takwimu zikionyesha matukio ya utapeli yakiongezeka huku hatua zikiendelea kuchukuliwa kuudhibiti.

Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) mwaka 2023 inaonyesha matukio ya uhalifu mtandaoni yaliongezeka, huku zaidi ya Sh5.06 bilioni zikitapeliwa kutoka kwa wananchi kupitia mitandao ya simu ikihusisha kuhamisha fedha kutoka benki au kutoa fedha taslimu.

Katika taarifa ya robo ya pili ya mwaka inayoandaliwa na TCRA inaitaja mikoa ya Rukwa, Morogoro, Mbeya na Dar es Salaam kuongoza kwa majaribio ya ulaghai na matukio ya uhalifu kwa njia ya mtandao.

Mei 15, 2024 Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na TCRA ilitangaza kuwakamata na kuwahoji watu 27 kwa tuhuma za makosa ya kimtandao yakiwamo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro alisema watuhumiwa hao walikuwa wakiwapigia simu watu na kusambaza ujumbe wakidai fedha imetumwa kimakosa, hivyo zirudishwe huku wakiwepo wengine wanaowadanganya watu kuwa wameshinda na kupata gawio kutoka kampuni za simu.

Akizungumza leo Ijumaa Novemba 22, 2024 Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema Serikali haiwezi kuvumilia kuona wananchi wanaendelea kutapeliwa na watu wachache ambao wamedhamiria kujinufaisha kupitia teknolojia.

“Kama kuna mtu yeyote anafikiria anaweza kutumia teknolojia kufanya ujanja wa kutapeli na kujipatia kipato kwa gharama ya nguvu za watu wengine, wakati huo umekwisha.

“Naelekeza Jeshi la Polisi na vyombo vya dola kwa ujumla kuelekeza nguvu katika yale maeneo ambayo yanaonekana kuwa sugu kwa utapeli, wakafumue mtandao wa wizi huu. Tumegundua uhalifu huu unakua kwa kasi kubwa, hivyo vita yake inapaswa kuwa kubwa,” amesema.

Masauni amesema pamoja na uratibu wa wizara hizo mbili, kikosi kazi hicho pia kitahusisha Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.

“Baada ya kikao hiki tumewaelekeza makatibu wakuu wa wizara hizi mbili wakae na kuwashirikisha makatibu wakuu wa wizara nyingine ambazo tunaona zinahusika kwa namna moja au nyingine na uhalifu mtandaoni pamoja na wadau ambao wanaweza kuwa na mchango katika teknolojia na kukabiliana na uhalifu ili kushughulikia changamoto hii ambayo imeanza kuwa sugu,” amesema.

Waziri Masauni amesisitiza wadau kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wajue umuhimu wa kujilinda wanapotumia mitandao na namna wanaweza kulinda taarifa zao binafsi zisifike kwa watu wenye nia ovu.

Amesema wizara itaendelea kuwekeza katika rasilimaliwatu yenye uwezo wa kukabiliana na aina hiyo ya uhalifu ikiwa ni pamoja na kuongeza vitendea kazi vinavyoendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia.

“Kwa upande wetu uwekezaji umeshaanza, kuanzia kwenye kutengeneza mifumo ya kushughulikia uhalifu wa aina hii hadi kuajiri vijana wenye ubobezi kwenye teknolojia na kuwaongezea uwezo waliopo kazini, haya yote yanaenda pamoja na kuwekeza kwenye vitendea kazi,” amesema.

Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Jerry Silaa amewataka wananchi kutoa taarifa za utapeli au ulaghai kwa Jeshi la Polisi ili hatua ziweze kuchukuliwa.

“Hakuna tukio la uhalifu wa kimtandao linaweza kufanyiwa kazi kama si mwananchi mwenyewe kutoa taarifa kwa vyombo husika, ikihusisha kutoa taarifa, kusaidia Jeshi la Polisi kwenye uchunguzi na kuisaidia Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwenye kukusanya ushahidi.

“Kingine muhimu wananchi kuwa na utaratibu wa kuhakiki namba zao ili kujiridhisha kuwa vitambulisho vyao vya Nida havijatumika kusajili namba nyingine. Pia wasikubali kupokea maelekezo kutoka kwa namba yoyote ya simu isipokuwa 100 ambayo inatumiwa na watoa huduma wote wa mawasiliano pindi wanapohitaji kuwasiliana na wateja wao,” amesema.

Waziri ametoa maelekezo kwa kampuni za simu kusimamia usajili wa laini za simu, kutumia alama za vidole kama inavyoagizwa na TCRA, kutoa elimu ya matumizi sahihi na salama ya huduma wanazozitoa kwa wateja wao.

Amezitaka kampuni hizo kutoa ushirikiano stahiki kwa wadau katika kushughulikia matukio ya uhalifu wa kimtandao yanapojitokeza.

“Kwenye kikao hiki tulikuwa na wadau wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambao tumekubaliana waendelee kuimarisha usimamizi wa mawakala wa huduma za kifedha ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kuongeza masharti katika utoaji wa fedha taslimu kwa mawakala wao.

“Pia tumewaomba Benki Kuu watoe elimu ya huduma za kifedha zinazotolewa mtandaoni na watoa huduma wasiosajiliwa, wananchi wanatakiwa kujua kwamba watoa huduma za fedha mtandaoni lazima wawe na usajili,” amesema.

Kwa upande wa Serikali, amesema wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa sera ya Tehama na kuifanyia maboresho pale itakapohitajika ili kuakisi mwenendo wa ukuaji wa sekta ya mawasiliano.

Sambamba na hilo, amesema wizara itaendelea kuratibu ushirikiano baina ya wadau wanaoshughulikia masuala ya usalama mtandaoni kwa lengo la kupambana na uhalifu katika eneo hilo.

Related Posts